Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Simon Simalenga amekemea
vikali vitendo vya baadhi ya wafugaji wilayani humo kuchungia mifugo ndani ya
Hifadhi hususani Pori la Akiba Maswa huku akisisitiza kuwa wilaya hiyo sio
sehemu salama kwa watu wanaofanya ujangili na wanaovunja sheria, kanuni na
taratibu zilizowekwa kwa ajili ya
kulinda rasilimali za nchi.
Akizungumza na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari
Februari 6, 2025 wilayani humo Mhe. Simalenga amesema vitendo hivyo vimekuwa
vikileta athari kubwa kwa mazingira ya hifadhi, na pia kuhatarisha usalama wa
wafugaji wanaoingia ndani ya hifadhi dhidi ya wanyamapori wakali pamoja na
kuharibu mfumo ikolojia wa maeneo hayo.
"Niwasihi sana wananchi wote walio ndani ya wilaya ya
Bariadi, maeneo ya Pori la Akiba Maswa, maeneo ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti
Kwa kipande kinachoingia wilaya ya Bariadi Kata ya matongo sio maeneo ya kwenda
kuchunga mifugo wala haifai kwenda kuingiza mifugo kwenye hayo maeneo,"
amesema Mhe. Simalenga.
Katika hatua nyingine Afisa Habari wa Mamlaka ya Usimamizi
wa Wanyamapori Tanzania - TAWA Beatus Maganja akiongea na wananchi wa Kijiji
cha Halawa wilayani humo wakati wa programu ya utoaji elimu amebainisha athari
mbalimbali zinazoweza kusababishwa na vitendo vya kuchungia mifugo ndani ya
hifadhi kuwa ni pamoja na ushindani wa malisho unaotokana na mwingiliano kati
ya wanyamapori na wanyama wafugwao ambao unaweza kupelekea wanyamapori kupoteza
maeneo yao ya asili ya kulisha au maji.
Maganja amebainisha kuwa wanyamapori wanapohisi tishio la
upungufu wa malisho yao ya asili wakati mwingine huhama katika maeneo hayo na
kuelekea maeneo mengine ikiwemo makazi ya watu na hivyo kupelekea migongano
kati ya binadamu na wanyamapori.
Naye CI Lusato Masinde Afisa Uelimishaji kutoka Kanda ya
ziwa ya TAWA amesema katika kuhakikisha usalama wa wananchi wa vijiji 32
vinavyozunguka hifadhi hiyo TAWA kupitia Pori la Akiba Maswa wamekuwa wakitoa
elimu ya mbinu za kukabiliana na
wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi hao ambapo katika kipindi cha kuanzia
Julai 2024 mpaka Januari 2025 wameweza kuwafikia wananchi zaidi ya elfu
arobaini na tano (45,000) wakiwemo wanafunzi wa shule mbalimbali.
Sambamba na hilo Masinde amesema TAWA imekuwa ikiwadhibiti
wanyamapori hao kwa kutumia nyenzo mbalimbali ikiwemo mabomu baridi waliyopokea
kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na hivyo matukio ya wanyamapori wakali na
waharibifu yameendelea kupungua siku hadi hadi siku.
Wananchi wa Kijiji cha Halawa wilayani Bariadi wamepongeza
jitihada zinazofanywa na TAWA katika kuwaelimisha masuala mbalimbali ya
uhifadhi ikiwemo athari za kuchungia mifugo ndani ya hifadhi na kukiri kuachana
na shughuli hizo kwani zimechangia kupata umasikini hasa pale wanapolazimika
kulipia faini mifugo inayokamatwa ndani ya hifadhi.
"Mimi nilikuwa na ng'ombe 30 ambazo nilikuwa
nazichungia ndani ya hifadhi ya Maswa, nikakamatwa na kulazimika kuuza ng'ombe
5 ili kulipa faini kuwakomboa ng'ombe waliobaki nikabaki na 25, kwahiyo
niliwapoteza ng'ombe watano Kwa ajili ya kuchungia hifadhini," amesema Ngomanzito
Lenhya Mkazi wa Kijiji cha Halawa.
"Tangu siku hiyo sitaki tena kuchungia hifadhini bora nitunze ng'ombe wangu 25 hao angalau na nyumba nijenge familia yangu ilale pazuri," ameongeza Ngomanzito.
Na. Mwandishi Wetu, Bariadi - Simiyu




0 Maoni