WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa madhehebu ya dini kuendelea kufundisha na kuimarisha elimu ya dini ili kutoa fursa kwa watoto na vijana kupata elimu hiyo na kuwaandaa kuwa watu wema.
Ametoa wito huo leo Jumapili (Februari 23, 2025)
alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha Tuzo
za 33 za Kimataifa za Kuhifadhi Qurani Tukufu. yanayofanyika katika uwanja wa
Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
“Jukumu la kuhakikisha maadili bora ni la kwetu sote,
madhehebu ya dini yakiwa na mchango mkubwa. ”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amehimiza madhehebu yote ya dini
kuendelea kuhubiri amani, mshikamano na utulivu hasa katika kipindi cha
kuelekea katika Uchaguzi Mkuu. “Amani na utulivu ni moja ya Tunu katika nchi
yetu,” alisisitiza Mheshimiwa Majaliwa.
Akizungumza kuhusu tuzo hizo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa yanatoa nafasi ya kujenga maadili bora ikiwemo uaminifu, umakini, na kujitolea. “Washiriki wanajifunza umoja, upendo na mshikamano na wengine kwa ufanisi.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa mashindano hayo
yanahamasisha jamii ya Kiislamu duniani kote kuwa na utamaduni wa kujisomea na
kuhifadhi Qur'aan Tukufu. “Hii inachangia kuendeleza utamaduni wa kuheshimu
dini, kudumisha maadili mema, amani na kuimarisha imani katika jamii”.
“Mashindano haya yanawawezesha vijana na watoto kuonesha
uwezo wao katika usomaji na uhifadhi wa Qur'aan Tukufu. Hii ni fursa muhimu
kwao kukuza kipaji, kujivunia mafanikio yao, na pia kujenga nidhamu na
uwajibikaji. ”
Ameongeza kuwa Serikali inaamini mashindano hayo yatasaidia
kuleta maendeleo ya kiroho kwa vijana na kuhamasisha jamii kwa ujumla.
“Serikali itaendelea kushirikiana na jumuiya na taasisi mbalimbali katika
kukuza na kuhamasisha shughuli za kidini”.
Naye, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar
Zuber Bin Ally amewataka waumini wa kiislam nchini kudumisha amani na kuepuka
kujiingiza katika viashiria vyovyote vinavyoweza kusababisha mmomonyoko wa
maadili. “Nchi yetu kote duniani inasifika kwa kutunza amani tuliyonayo,
tuendelee na utamaduni huu. ”
Mashindano hayo yameandaliwa na Jumuiya ya kuhifadhisha
Qur'an Tanzania ambayo yanalenga kutoa fursa kwa Waislamu kutoka sehemu
mbalimbali duniani kuonesha uwezo wao katika kuhifadhi na kusoma Qur’an Tukufu
kwa usahihi na umakini mkubwa.
Washindi wa tuzo hiyo kwa washiriki wenye umri zaidi ya
miaka ishirini ni Mohamed Amin Hassan mshindi wa kwanza kutoka nchini Marekani,
Ismail Ally mshindi wa pili kutoka Kutoka nchini Libya na Malik AbdulAzizi
mshindi wa tatu kutoka nchini Saudi Arabia.
0 Maoni