Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo
na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Kuendeleza Nishati ya Jua
(ISA), Dkt. Ajay Mathur yenye Makao Makuu yake nchini India ambaye ameeleza nia
ya ISA kuwekeza katika miradi ya umeme jua nchini.
Mazungumzo kati ya Dkt. Biteko na Dkt. Mathur
yamefanyika jijini New Delhi nchini India ambapo Dkt. Biteko alishiriki Wiki ya
Nishati India ambayo ilienda sambamba na mikutano mbalimbali kuhusu nishati.
“ Tunawaalika mje kuwekeza Tanzania kwani
tunahitaji kuwa na miradi mingi ya umeme kutoka vyanzo tofauti ili kuweza
kutosheleza mahitaji ya watu wetu na kinachotupa msukumo zaidi kwa sasa ni mpango
mahsusi wa misheni 300 tuliousaini mwezi Januari 2025 ambapo Tanzania tunapaswa
kupeleka umeme kwa wananchi milioni 8.3 ifikapo mwaka 2030,” amesema Biteko.
Dkt. Biteko
ameishukuru Taasisi ya ISA kwa kuona Tanzania kama sehemu sahihi ya uwekezaji
na kueleza kuwa kazi yake ni kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na miradi mingi ya
nishati ambayo italeta utoshelevu wa umeme na kuchagiza maendeleo huku
akisisitiza kuwa suala la kuwa na umeme wa kutosha si la kusubiri miradi
inapaswa kutekelezwa sasa.
Kuhusu miradi
ya umeme Jua nchini, Dkt. Biteko amesema Tanzania imeanza kutekeleza mradi wa
umeme jua wa megawati 150 wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kwa kuanza na
megawati 50 ambapo megawati 100 zitaanza kutekelezwa baada ya kukamilika kwa
awamu ya kwanza.
Ameongeza
kuwa, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pia limepata maeneo matatu kwa ajili
ya miradi ya umeme jua ambayo ni Zuzu, Dodoma (MW 60), Mkwese, Manyoni -
Singida (MW 199) na Same, Kilimanjaro (MW 50) ambapo ameishukuru ISA kwa
kukubali kufanya upembuzi wa awali katika maeneo hayo.
Ili kuwezesha
uwekezaji wa Taasisi hiyo nchini, Dkt. Biteko amewataka Watendaji hao kuainisha
maeneo ambayo wanahitaji kuwekeza ili Wataalam waanze kuyafanyia kazi.
Awali,
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya ISA, Dkt. Ajay Mathur alimweleza Dkt.Biteko
kuwa Taasisi hiyo inataka kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya umeme jua nchini
huku msukumo wakiupata pia kutoka kwenye Mkutano wa Misheni 300 ambao ulieleza
nia ya Afrika kufikisha umeme kwa watu milioni 300 Tanzania ikiwemo.
Amesema
Taasisi ya ISA inafanya kazi kwenye nchi 122 duniani na inashirikiana na
Serikali mbambali katika utekelezaji wa miradi ya umeme jua kwa njia mbalimbali
ikiwemo kutoa mafunzo kwa wazawa kuhusu utengenezaji wa vifaa vya umeme jua,
kusaidia serikali kutengeneza sera zinazowezesha uwekezaji katika nishati ya
jua, kuwajengea uwezo wahandisi wa nishati ya jua na watunga sera za nishati
katika maeneo mbalimbali yanayohusu uendelezaji wa Nishati ya Jua.
Katika hatua
nyingine, Mathur amesema kuwa tayari Taasisi ya ISA imeanza kufanya kazi
Tanzania kwa kuanzisha Kituo cha Uendelezaji wa Teknolojia ya Nishati ya Jua
(Solar Technology Applications Resource Center
- STAR-C) ambacho kitakuwa na majukumu mbalimbali ikiwemo uendelezaji
wataalam wa ndani ya nchi na kufanya tafiti ambazo zitasaidia Utekelezaji wa
miradi ya Nishati jua kwa kuzingatia Mazingira ya nchi yetu, kuandaa mitaala,
kufanya ukarabati na ujenzi wa majengo ya maabara kwa ajili ya tafiti na
kufundishia, ununuzi wa vifaa kwa ajili ya kufundishia na upimaji wa viwango
vya ubora wa vifaa vya Umeme Jua.
Vilevile
kituo hicho kitasaidia ubunifu wa bidhaa na huduma zinazohimiza matumizi ya
nishati ya jua, pamoja na kusaidia biashara katika mnyororo wa thamani wa sekta
hiyo.
Ameongeza
kuwa, kituo hicho ambacho kimejengwa katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC)
kitazinduliwa mwezi Juni mwaka huu.
Kwa Afrika, ISA imeanzisha vituo vya STAR C
nchini Uganda, Ethiopia, Somalia, Ivory Coast na Ghana ambapo tangu kuanzishwa
kwake vituo hivyo vimefundisha maelfu ya wataalam katika sekta ya nishati ya
jua.
Mazungumzo
kati ya Dkt. Biteko na Dkt. Mathur yalihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini
India, Mhe. Anisa Mbega na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu,
Mhandisi Innocent Luoga.
0 Maoni