WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa amezielekeza mamlaka za mikoa, halmashauri na taasisi za elimu
nchini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014
Toleo la mwaka 2023, kwa ufanisi kulingana na majukumu yao.
Pia,
Mheshimiwa Majaliwa amezitaka halmashauri ziweke kipaumbele katika kuanzisha na
kuendesha shule za amali ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kuajiriwa au
kujiajiri na hatimaye kuchangia katika maendeleo ya Taifa letu.
Ametoa
maelekezo hayo leo Ijumaa (Februari 14, 2025) wakati akisoma hotuba ya
kuahirisha Mkutano wa 18 wa Bunge la 12, bungeni jijini Dodoma.
“Sera na
Mitaala hiyo ni maono na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
yenye lengo la kufanya elimu inayotolewa hapa nchini iwiane na mahitaji ya
sasa, lakini pia wahitimu wapate stadi na maarifa yatakayomudu mabadiliko na
kasi ya ukuaji wa teknolojia.”
Katika hatua
nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa hali ya uzalishaji na upatikanaji wa
chakula nchini imeendelea kuimarika ambapo katika msimu wa 2023/2024 uzalishaji
wa mazao ya chakula ulifikia tani milioni 22.8.
“Kwa
kuzingatia uzalishaji huo na mahitaji ya chakula ya tani milioni 17.7 kwa mwaka
2024/2025, nchi itakuwa na utoshelevu wa asilimia 128. Hadi kufikia tarehe 31
Januari, 2025 Wakala imehifadhi jumla ya tani 776,000 za nafaka katika ghala za
Wakala zilizopo kwenye maeneo mbalimbali nchini.”
Kadhalika,
Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wananchi wanaoishi kwenye baadhi ya maeneo
nchini yanayopata mvua chache kuchukua tahadhari mapema na kuzalisha mazao
yanayokomaa kwa muda mfupi. “Hatua hii iende sambamba na kutumia vizuri mavuno
yaliyopatikana kwa kutunza chakula cha kutosha katika ngazi ya kaya.”
Akizungumzia
kuhusu tuzo maalum ya Kimataifa ya The Global Goalkeeper Award aliyopewa Rais
Dkt. Samia kutoka Taasisi ya Gates, Mheshimiwa Majaliwa amesema tuzo hiyo ni
kielelezo cha utashi wake katika kuharakisha malengo ya maendeleo endelevu nchini.
Pamoja na
mambo mengine, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amepewa tuzo hiyo kutokana na
jitihada alizozifanya katika kupunguza viwango vya vifo vya wajawazito na
watoto chini miaka mitano lakini pia kukabiliana na tatizo la udumavu.
Mheshimiwa
Majaliwa amesema kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kiwango cha vifo vinavyotokana
na uzazi vimepungua kutoka vifo 556 mwaka 2015 hadi vifo 104 mwaka 2022 kwa
kila vizazi hai 100,000. Idadi hiyo nisawa na asilimia 80.
Pia,
Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa rai kwa wafanyabiashara wote kutopandisha bei za
vyakula kiholela wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
“Wafanyabiashara wote watambue ya kwamba mchango wao ni muhimu katika
kufanikisha ibada hii, ninawasihi sana endeleeni kushiriki katika ibada hii kwa
kurahisisha upatikanaji wa bidhaa muhimu.”
Bunge
limeahirishwa hadi siku ya Jumanne Aprili 08, 2025.
0 Maoni