Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Vipimo (WMA) imekagua Jengo la Ofisi Kuu ya Wakala hiyo lililo katika hatua za mwisho kukamilika na kukiri kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika ujenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo ya
ukaguzi iliyofanyika leo Februari 7, 2025 jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Bodi,
Prof. Eliza Mwakasangula amesema hatua iliyofikiwa katika ujenzi husika,
inadhihirisha pasipo shaka kuwa litakabidhiwa katika hali ya ukamilifu hapo
Februari 10, mwaka huu kama inavyotarajiwa.
“Tumeridhishwa sana na kazi iliyofanywa na Mkandarasi kwa
kushirikiana na Mshauri Elekezi. Kinachofanyika sasa ni kukamilisha kazi ndogo
ndogo zilizosalia. Kwa hatua iliyofikiwa, hatuna shaka kufikia tarehe 10 mwezi
huu, ambayo ndiyo siku ya kukabidhiwa rasmi, Jengo litakuwa limekamilika kwa
viwango stahiki,” amesema.
Aidha, Prof. Mwakasangula amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kutenga bajeti ya ujenzi wa Jengo hilo ambalo limegharimu takribani
shilingi bilioni 6.2 ambazo ni fedha za ndani.
Pia, amemshukuru Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.
Selemani Jafo na Menejimenti yake pamoja na kumpongeza Mtendaji Mkuu wa WMA,
Alban Kihulla na Menejimenti yake yote kwa usimamizi mzuri wa jengo hilo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu Kihulla amewaeleza waandishi
wa habari kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutatatua changamoto mbalimbali za
kiofisi.
“Tumeanza na jengo hili lakini matarajio ni kujenga katika
maeneo mengine ili mazingira ya kiofisi kwa wateja wanaokuja kupata huduma yawe
mazuri lakini na kwa watumishi pia.”
Ametaja faida nyingine ya kukamilika kwa jengo hilo kuwa ni
kuwezesha vifaa vya kitaalamu kukaa katika mazingira ambayo ni mazuri ili
kuendana na usahihi wa kimataifa.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Ukandarasi ya Mohamed Builders
inayojenga jengo hilo, Jaffar Mohamed amemhakikishia Mwenyekiti na Wajumbe wa
Bodi hiyo kuwa watakabidhi jengo hilo likiwa limekamilika Februari 10 mwaka huu
kama ilivyopangwa.
Wafanyakazi wa Wakala wa Vipimo Makao Makuu, ambao kwa sasa wako Dar es Salaam, wanatarajiwa kuhamia Dodoma hivi karibuni baada ya kukamilika kwa Jengo hilo ikiwa ni kutimiza maelekezo ya Serikali yanayozitaka Taasisi na Mashirika yote ya Umma kuhamia Makao Makuu ya nchi, Dodoma.
Na. Veronica Simba - WMA


0 Maoni