Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila imeendelea kujikita katika
kutoa huduma za ubingwa bobezi ambapo leo imewaruhusu wagonjwa watano na
kufikisha idadi ya wagonjwa waliofanyiwa upandikizaji kufikia 15 tangu huduma
hiyo ilipoanzishwa hospitali hapo mwaka 2023.
Akiongea na Waandishi wa habari wakati wa kuwaruhusu
wagonjwa hao kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Naibu Mkurugenzi Mtendaji
MNH-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema kutolewa kwa huduma hizo ni matokeo
ya uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Magandi ameongeza kuwa hakuna sababu ya Watanzania
kwenda nje ya nchi kwa huduma za upandikizaji figo kwakuwa wataalam wa ndani
wana uwezo wa kutoa huduma hizo kwani wana weledi wa kutosha, miundombinu
wezeshi, vifaa tiba na mazingira mazuri ya kutolea huduma.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo MNH
Mloganzila Dkt. Immaculate Goima amesema hospitali hiyo ina wagonjwa takribani
90 ambao wanapatiwa huduma za kusafisha damu, ambapo kati ya hao 60 wanahitaji
upandikizaji figo lakini hawajapata wa kuwachangia hivyo amewashauri ndugu zao
kujitokeza kufanya vipimo na kuwachangia ndugu zao figo ili kuwaondolea changamoto wanazopitia.
Naye, Daktari Bingwa wa Upasuaji Mfumo wa Mkojo Dkt. Hamis
Isaka amesema teknolojia iliyotumika kuvuna figo ni ya kisasa ya kutumia
matundu madogo (Hand Assisted Laparoscopic Donor Nephrectomy) ambapo mtoa figo
anakaa hospitalini siku mbili hadi tatu na kurudi katika majukumu yake kati ya
wiki mbili hadi nne.
Mmoja wa wanufaika wa huduma hiyo amewashukuru wataalam wa hospitali hiyo kwa huduma nzuri za matibabu, ushauri, upendo na ufuatiliaji uliokuwa ukifanywa na wataalam hao kabla na baada ya kupandikizwa figo ambapo kwao imewapa faraja kubwa sana.

0 Maoni