Serikali kupitia Wizara ya Madini inaendelea na juhudi za
kupunguza mzigo wa tozo kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu hapa nchini kwa
kufanya mapitio ya ada na ushuru mbalimbali unaotozwa katika mnyororo wa
uchimbaji na uchenjuaji wa madini hayo.
Hatua hiyo imebainishwa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony
Mavunde, leo Februari 7, 2025, Bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la
Mbunge wa Jimbo la Busanda, Mhe. Tumaini Magessa ambaye alitaka kujua ni lini
Serikali itapitia upya tozo zilizopo kwenye mnyororo wa uchimbaji na uchenjuaji
wa dhahabu zinazowaelemea Wachimbaji Wadogo.
Katika majibu yake, Waziri Mavunde amesema kuwa kupitia
Mkakati wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI), Wizara ya Madini imefanya
utafiti wa tozo 66 zinazotozwa na Halmashauri mbalimbali katika shughuli za
uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu na kutaja baadhi ya tozo hizo kuwa ni ushuru
wa karasha, ada ya ukaguzi, kodi ya ongezeko la thamani (VAT in leaching/CIP),
ushuru wa kusafirisha miamba ya madini, na visusi (mabaki ya miamba baada ya
uchenjuaji).
“Katika kutatua changamoto hizi, Wizara iliitisha kikao
Mwezi Agosti, 2024 Mkoani Singida ambacho kilishirikisha Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Wizara ya Fedha, Tume ya Madini,
STAMICO, Halmashauri za Wilaya (Ikungi, Chunya, Kahama, Msalala, Meatu,
Shinyanga, Mtama na Lindi), FEMATA na TAWOMA. Rasimu ya Mapendekezo ya
Maboresho tayari imeshaandaliwa na ipo katika hatua ya kufanyiwa mapitio na
tathmini, ambapo Matokeo ya tathmini hiyo yatatusaidia katika kupanga tozo
rafiki kwa wachimbaji wadogo,” amesema Mhe. Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde ameongeza kuwa, Serikali inaendelea na
maboresho makubwa ya mfumo wa kodi kupitia Tume ya Maboresho ya Kodi
iliyoanzishwa na Mhe. Rais. Dkt. Sa,mia Suluhu Hassan na kwamba tume hiyo
inatarajiwa kutoa mapendekezo yatakayosaidia kupunguza changamoto za kikodi
zinazowakabili Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu na Sekta ya Madini kwa ujumla.
Hatua hizo zinadhihirisha dhamira ya Serikali katika kuboresha mazingira ya uchimbaji mdogo wa madini na kukuza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi.

0 Maoni