Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA)
inashiriki mkutano wa kimataifa wa Utalii na Usafirishaji unaofanyika Dubai,
Falme za Kiarabu ambao umeanza tarehe 15/01/2025 na unatarajia kumalizika leo
tarehe 16/01/2025.
Mkutano huo ambao
umeandaliwa na Taasisi ya Teknolojia na Utafiti ya barani Asia (ITAR)
unahudhuriwa na washiriki kutoka takribani nchi 52 duniani kote.
Katika Mkutano huo ambao unalenga kuonyesha mapinduzi ya
kiteknolojia katika tasnia ya utalii na usafirishaji na kubadilishana mawazo
baina ya washiriki wa mkutano huo kwa ajili ya kuboresha sekta ya utalii na
usafirishaji, TAWA inawakilishwa na Mhifadhi Mwandamizi Kelvin Fella ambaye ni
Kamanda wa Hifadhi ya Magofu ya Kilwa.
Kupitia Mkutano huo SC. Kelvin Fella amefanya wasilisho
kuhusu namna miundombinu ya kitalii na usafirishaji iliyofanywa na TAWA
inavyosaidia ukuaji wa utalii katika Hifadhi ya Kilwa.
Aidha SC. Fella aliezea kuhusu umuhimu wa Hifadhi ya
Kilwa Kisiwani na Songomnara ambayo ni Urithi wa Dunia na kuwasilisha shughuli za utalii
zinazofanyika Kilwa pamoja na kuwakaribisha wageni kutoka mataifa mbalimbali
kutembelea Kilwa na Tanzania kwa ujumla.
Mbali na kuelezea utalii wa Kilwa SC. Fella alitangaza
shughuli za utalii katika maeneo mengine yanayosimamiwa na TAWA pamoja na fursa
za uwekezaji katika shughuli za utalii wa uwindaji na kugawa vipeperushi kwa
washiriki wa mkutano huo. Aidha aliwasihi washiriki hao kuchangamkia fursa hizo
na kuwa mabalozi wazuri wa TAWA.


0 Maoni