MKUU wa Wilaya ya Mbogwe Mheshimiwa Sakina Jumanne amekabidhi
hundi ya Fedha Shilingi Milioni 500 kwa Wanawake, Vijana na Makundi Maalum.
Fedha hizo ni sehemu
ya Shilingi Milioni 800 zilizotengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe
kutolewa kama mkopo wa Asilimia 10 ya Mapato ya ndani.
Akizungumza leo
Januari 16, 2025 Sakina amesema makundi yaliyopewa mikopo ni pamoja na
kundi la vijana ambapo kwa namna ya tofauti vijana wamekabidhiwa pikipiki 20
ili wafanye shughuli za ujasiriamali na kujiletea maendeleo.
Aidha, Sakina amewataka wananchi wa Mbogwe kutambua kazi
kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwaletea wananchi
maendeleo ambapo katika mwaka wa fedha 2024/2024 Mbogwe imetenga jumla ya
Milioni 800 kwenda kwa wananchi kujiletea maendeleo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amewataka watumishi wa Halmashauri ya Mbogwe hususan Idara ya
Maendeleo ya Jamii kuelimisha wananchi kujiunga kwenye vikundi ili
wanufaike na fedha zilizotengwa kutolewa kwa wananchi kama mkopo kwani kama
hawatawaelimisha wananchi na kuwasaidia kujisajili kwenye mfumo, fedha nyingi
zitakosa wakopaji wenye sifa.


0 Maoni