Serikali imesema kuwa itaendelea kushirikiana na Shirika
la Fedha la Kimataifa (IMF), na kuhakikisha Fedha zote za maendeleo
zinazotolewa na Shirika hilo zinatumika kukamilisha azma ya kukuza uchumi wa
nchi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu
Lameck Nchemba (Mb), jijini Dodoma wakati akimuaga Kiongozi wa Timu ya Wataalam
ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa Tanzania, Bw. Charalambos
Tsangarides, aliyemaliza muda wake baada ya kuhudumu kwa zaidi ya miaka mitatu
na nusu.
Alisema Serikali itaendelea kutekeleza dhamira yake ya
kuwaletea wananchi maendeleo na kukuza uchumi kwa ujumla kupitia juhudi
mbalimbali inazofanya ikiwemo kutafuta fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya
kimkakati.
‘Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, napenda kutoa
shukrani zetu za dhati kwa kujitolea kwako katika kusaidia safari ya maendeleo
ya kiuchumi ya nchi yetu, ninawahakikishia kwamba Timu yangu itawapa
ushirikiano wote unaohitajika, kwa upande mwingine, nina furaha kuwajulisha
kwamba tunaendelea vyema na hatua zetu za mageuzi chini ya program mpya ya
Serikali ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la
Resilient and Sustainable Fund (RSF),’’ alisema Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba, mbali na kumuaga Kiongozi huyo wa IMF nchini,
alitumia fursa hiyo kumkaribisha Kiongozi mpya anayechukua nafasi hiyo Bw.
Nicolas Blancher, huku akimuahidi ushirikiano kutoka Serikali ya Tanzania.
‘’Napenda kuchukua fursa hii kumkaribisha rasmi Bw.
Nicolas Blancher, kama Kiongozi wetu mpya wa “Mission” kwa Tanzania na
tunafurahi kupata nafasi ya kushuhudia mwongozo kutoka kwa mtaalamu mwingine
kama tulivyofanya na Kiongozi wa “Mission”anayemaliza muda wake katika
kufanikisha maendeleo yetu endelevu ya kiuchumi’’ alisema Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake Kiongozi wa Timu ya Wataalam ya Shirika
la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa Tanzania, anayemaliza muda wake, Bw.
Charalambos Tsangarides, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano
mkubwa alioupata wakati akitekeleza majukumu yake nchini.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa juhudi za kusimamia
maendeleo ya kiuchumi na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika
kuimarisha ustawi wa wananchi wake hata baada ya kumaliza muda wake wa
kuhudumu.
Naye Kiongozi Mpya wa Timu ya Wataalam ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bw. Nicolas Blancher, ameahidi kushirikiana kikamilifu na Serikali ya Tanzania na kumhakikishia Dkt. Nchemba kuwa ataendeleza ushirikiano na kazi zilizofanywa na mtangulizi wake huku akisisitiza dhamira ya kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanatimia.
Na. Saidina Msangi na Asia Singano- WF, Dodoma


0 Maoni