Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) jana Januari 20, 2025 limeendesha mafunzo maalum kwa Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) jinsi ya kudhibiti mioto kichaa inayotokea ndani ya Hifadhi za Taifa inayosababishwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu kama vile ujangili na utayarishaji wa mashamba unaotekeleza na wananchi wanaopakana na hifadhi hizo.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa Mikumi
kwa Wanajeshi wa Kikosi cha Usafiri wa Anga 603 KJ kutoka Dar es Salaam
yalilenga kuleta ufanisi wakati wa kukabiliana na majanga ya moto yanapotokea
ndani na nje ya Hifadhi za Taifa Tanzania.
Akitoa mafunzo hayo kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi -
TANAPA, Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza Samwel Mgohach alisema, “Mioto Kichaa
ni moja ya changamoto zinazotukabili katika hifadhi zetu kwani huathiri viumbe
hai wengi sana hususani wale wanaotambaa na wanyama wenye mimba na wale wenye
ndama wadogo ambao hawawezi kukimbia kipindi moto unapochachamaa.”
Aidha, mioto hii pia imeendelea kuathiri ikolojia ya
hifadhi na maeneo yaliyohifadhiwa na kusababisha baadhi ya viumbe kutoweka
katika ardhi ya Tanzania, hata hivyo mioto hii huongeza kasi ya mabadiliko ya
tabianchi ambayo madhara yake ni pamoja na ukame, kuongezeka kwa joto duniani
na matetemeko ya ardhi, aliongeza Afisa Uhifadhi Mgoach.
Mioto ambayo imeendelea kulikumba Shirika la Hifadhi za
Taifa Tanzania na maeneo mengine nchini ni pamoja na “surface fire” ambao
husambaa juu ya tabaka la ardhi kwa kuunguza majani na nyasi lakini hauna
madhara makubwa kwa mizizi na tabaka la udongo, aina nyingine ni “Crown fire na
Ground fire” ambao hutambaa chini kwa ukiathiri mizizi na mashina ya miti.
Mioto inayosambaa kwa mfumo huu husababishwa na
mkusanyiko wa mboji unaotokana na kudondoka kwa majani na kutengeneza tabaka
lingine la ardhi. Eneo linalokumbwa na kadhia ya moto wa aina ya “ground fire”
hususani nyakati za kiangazi ni Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro.
Ili kukabiliana na majanga ya mioto kwa haraka na kuokoa
maisha ya viumbe hao adimu dunia, Wanajeshi hao kutoka JWTZ pia, walipewa mbinu
za kisasa za kuutambua moto umbali ulipo kwa kutumia teknolojia ya “Satellite”
na kuzima moto kwa kutumia ndege nyuki almaarufu “Drones”.
Vile vile, Afisa Uhifadhi - Mgohach alieleza umuhimu wa kutumia moto ujulikanao kama
“Early Burning”kama njia ya kudhibiti mimea vamizi kama vile (Lantana camara),
kuboresha rutuba ya udongo, na kuua vimelea vya mayai ya wadudu waletao
magonjwa kwa wanyamapori.
Moto huu wa “early burning”unaotumiwa na wahifadhi wetu
pia umesaidia kurejesha wanyamapori ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa na
kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na binadamu kwani nyasi zikiwa ndefu
sana haziliwi na wanyama na kusababisha watoke hifadhini na kwenda maeneo yenye
nyasi fupi.
Naye, Meja Samson Ngowe kwa niaba ya Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), aliwashukuru TANAPA kwa mafunzo hayo na kuahidi kuendeleza
ushirikiano uliopo wa muda mrefu kati ya JWTZ na TANAPA katika nyanja
mbalimbali zikiwemo mafunzo, ushirikiano
wakati wa kupandisha Bendera ya Taifa na Mwenge wa Uhuru katika kilele cha
Mlima Kilimanjaro na kwenye majanga ya moto katika maeneo mbalimbali.
Pamoja na mafunzo hayo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pia lilipata fursa ya
kutembelea vivutio mbalimbali vilivyomo ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi na
kuridhishwa na namna ambavyo TANAPA wameendelea kuwa vinara wa uhifadhi nchini
na vivutio vyao kuwa ni kimbilio kwa watalii wengi kutoka ndani na
nje ya Tanzania.
Na. Zainab Ally - Mikumi.



0 Maoni