Kamishna wa Uhifadhi, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania
(TANAPA) Musa Kuji amefungua kikao kazi cha Maandalizi ya bajeti ya Mapato na
Matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kikao kinachofanyika katika Ukumbi wa
Mikutano wa Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara uliopo eneo la Mto wa Mbu mkoani
Manyara.
Kikao hicho cha siku mbili kilichoanza leo Januari 27, 2025
na kutarajia kutamatika tarehe 28.01.2025 kimelenga kufanya tathmini ya bajeti
iliyopita ya mwaka wa fedha 2023/2024 na kutathmini mwenendo wa bajeti
inayoelekea ukingoni ya mwaka huu wa fedha 2024/2025.
Hata hivyo wajumbe wa kikao hicho pia watajadili na
kupitisha mapendekezo yatakayotumika kuandaa bajeti ya Mapato na Matumizi kwa
mwaka mpya wa fedha 2025/2026 ili kuendana na kasi ya ukuaji wa sekta ya
uhifadhi na utalii nchini.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho Kamishna kuji
alisema “Kikao kazi hiki ni muhimu kwani kitawajengea uwezo wa kuandaa bajeti
inayotekelezeka kulingana na vipaumbele vya shirika huku ikiakisi matamanio ya
Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha Uhifadhi na Utalii.
Kikao kazi hicho cha maandalizi ya bajeti ya mwaka 2025/2026 kinachoendelea Ziwa Manyara ni hatua muhimu ya maandalizi ya rasilimali fedha zitakazotumika kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vitendea kazi vitakavyotumika kuimarisha Uhifadhi na kukuza Utalii kwa ajili ya mustakabali wa taifa letu.
Na. Philipo Hassan - Manyara



0 Maoni