Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Maxmillian Iranqhe amezindua
mitambo maalum na malori mawili mapya, yaliyonunuliwa na Halmashauri hiyo
kwaajili ya ukarabati wa barabara za mitaa ya Jiji hilo, akitoa wito wa matunzo
ya mitambo hiyo ili iweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu.
Wakati wa uzinduzi huo jana, Mhe. Iranqhe mbele ya Wananchi
wa Jiji la Arusha ameelekeza pia Kila Kata kukabidhiwa Shilingi Milioni 4,
kwaajili ya manunuzi ya vifusi vya kujengea barabara hizo, ikiwa ni fedha baki
kwenye bajeti ya Shilingi Bilioni 2 zilizokuwa zimetengwa awali kwenye manunuzi
ya Mitambo ya ujenzi wa barabara hizo.
Katika hatua nyingine, Mstahiki meya pia amehimiza suala la
utunzaji wa mazingira, akiwasihi madiwani kusimamia ajenda hiyo ya upandaji wa
miti kwa wingi hasa katika maeneo yanayokumbwa na ukame huku pia
akitahadharisha kuhusu ongezeko kubwa la utupaji wa taka mitaani hasa chupa za
Plastiki zinazozagaa kwenye mitaro na maeneo mbalimbali ya wazi suala
linalodumaza sifa ya Mkoa wa Arusha kuwa Kitovu cha Utalii kwa Tanzania bara.
Awali katika maelezo yake, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Ndugu John Kayombo kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi Mhe. Iranqhe, amesema mitambo hiyo itakwenda kujenga na kukarabati barabara za mitaa yote 154, akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Makonda kwa usimamizi na ufuatiliaji mzuri wa kuhakikisha Arusha inanufaika na miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
0 Maoni