Serikali imetoa kiasi
cha shilingi milioni 900 kwa ajili ya kuondoa vikwazo katika Barabara wilayani
Songea kwa ujenzi wa daraja la Mto Lumecha na kufungua barabara ya kilomita 4
katika kata ya Mkongotema sambamba na ujenzi wa daraja la Mto Liweta iliyopo
katika Kata ya Mpandangindo.
Meneja wa Wakala ya
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani humo, Mhandisi Bakari John,
ameeleza kuwa hizo ni juhudi za kuboresha miundombinu ya barabara zikilenga
kuinua uchumi wa wakulima wa Wilaya ya Songea kupitia mradi wa RISE programu ya
Uondoaji Vikwazo katika Barabara (bottleneck) iliyopo chini ya TARURA.
“Wananchi wa Mkongotema
na Mpandangindo, ambao ni wakulima wa mazao ya biashara kama tangawizi, mahindi
na parachichi, walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kusafirisha mazao yao
kutoka mashambani hadi sokoni”.
“Kukosekana kwa
miundombinu bora kulisababisha gharama za usafirishaji kuwa juu na kupunguza
faida kwa wakulima. Ujenzi wa madaraja na barabara umeleta mabadiliko makubwa,
na sasa wakulima wanaweza kufikisha mazao yao sokoni kwa urahisi,” amefafanua
Aidha, amesema kuwa
katika kipindi cha miaka minne ya Awamu ya Sita, Wilaya ya Songea imefanikiwa
kufungua barabara mpya zenye urefu wa kilomita 192 na kuongeza kuwa barabara
hizo zimeelekezwa mashambani, hatua inayolenga kuchochea uzalishaji na
kurahisisha usafirishaji wa mazao.
Mhandisi Bakari
ameongeza kuwa madaraja makubwa 6 yenye urefu wa zaidi ya mita 25 yamejengwa,
huku madaraja madogo zaidi ya kumi (10). “Miundombinu hii imekuwa mkombozi kwa
wakulima na jamii kwa ujumla, ikirahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii”.
Hata hivyo Mhandisi
Bakari amesisitiza umuhimu wa kutunza miundombinu hiyo kwa kuwa serikali
inatumia fedha nyingi kuijenga. “Ni wajibu wetu kuilinda ili iweze kuwanufaisha
vizazi vijavyo,” amesema.
Naye, Bw. Edsnon Lunji
mkazi wa Madaba-Mkongotema amesema zamani hawakuwa na barabara bali kulikua na
njia ya kutembea kwa miguu na magari yalikuwa yanazunguka umbali mrefu ambapo
gharama yake ilikuwa ni kubwa sana, hivyo anaishukuru serikali kwa kuwachongea
barabara na ujenzi wa daraja kwani kwa sasa itawarahisishia usafirishaji wa
mazao.
Kwa upande wake Bw.
Baitan Nyoni mkazi wa Mkongotema amesema
barabara hiyo inakuwa ni ya mkato na ameishukuru serikali kwa kuwaona kwani
sasa watasafirisha mazao yao kwa gharama nafuu na hata mara mbili kwa siku,
amesema awali walikuwa wakitumia kivuko cha miti ambapo watu wengi walidumbukia
mtoni na kuhatarisha maisha yao.



0 Maoni