Waziri wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde amesema Serikali imejidhatiti kurudisha hadhi ya Tanzanite kwa kufanya minada ndani na nje ya nchi ili kuyaongezea thamani na wafanyabiashara waweze kunufaika na kuongeza pato la taifa kwa ujumla.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Desemba 14, 2024
Mirerani mkoani Manyara wakati akizindua mnada wa madini ya vito ambao mara ya
mwisho ulifanyika mwaka 2017.
Mheshimiwa Mavunde amesema mojawapo ya maeneo
yanayosaidia kuongeza mapato ni pamoja na kudhibiti biashara ya madini, kuzuia
utoroshaji na kuifanya biashara hiyo kuwa katika mfumo sahihi, uwepo wa minada
utachochea uongezaji thamani ya madini ya vito.
“Madini ya Vito
yananunuliwa kwa asilimia kubwa kwa ajili ya ‘luxury’ ni ufahari na madini ya vito tunashindana na watu wengine
ndio maana Serikali inaendelea kuchukua hatua, tunarudisha hadhi ya Tanzanite
ili ikashindane vizuri duniani,”amesema Waziri
Mheshimiwa Mavunde na kuongeza,
“Moja ya hatua ya kwanza ni urejeshaji wa minada ya ndani
na ya kimataifa, ili tuyape thamani madini yetu, duniani kuna madini mengi ya
vito, moja ya sifa kubwa ya madini ya vito ni uadimu, Tanzanite ina sifa
hizo; Ila sio madini pekee yake
adimu, kuna nchi nyingine zina madini
adimu ambayo hayapatikani popote hivyo tunashindana kimataifa ni lazima
tuchukue hatua kuhakikisha tunarudisha hadhi ya Tanzanite katika soko la
kimataifa ili na bei iweze kuongezeka na wafanyabiashara wanufaike,”amesisitiza
Waziri Mavunde.
Amesema, katika vipengele (category) vya mawe duniani, jiwe
linaanzia kuwa Precious, semi-Precious halafu baadaye linakuwa jiwe la kawaida
na kwamba wanachukua hatua za makusudi ili Tanzanite lisiwe jiwe la kawaida.
“Tukiacha liwe la kawaida mtanunua kwa kilo kwa gharama
ndogo sana na mtashusha hadhi ya Tanzanite, Serikali haipo tayari kuona hilo
linatokea ndio maana tunayafanya haya kwa ajili ya kuhakikisha tunalinda hadhi
na heshima ya jiwe letu hili,” Amesisitiza Mheshimiwa Mavunde.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amewahakikishia
wadau wa madini kuwa Serikali haitachukua madini ya mtu baada ya mnada wa leo
na kama kuna madini yatabaki yatakabidhiwa kwa wahusika.
“Kumekuwepo na hisia na dhana baada ya mnada Serikali
itachukua madini yaliyobaki kwa sababu katika mnada wa mwisho wa mwaka 2017
kuna madini yalibaki na wahusika hawakurejeshewa mpaka leo, nataka
niwahakikishie Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan, itaendelea kusimamia kuhakikisha katika biashara hii pia tuwajengee
‘confidence’ mtafanye biashara kwa uhuru na hakuna namna yoyote kuwa serikali
itawaingilia na kuja kuyachukua madini yenu.
“Yale madini yaliyochukuliwa yapo, yalibaki Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) tumeshayatoa na tutawakabidhi rasmi wahusika ili waendelee na
biashara yao ya madini, nataka niwatoe hofu na muwe na amani,”amesema Waziri
Mavunde.
“Manyara tayari mna eneo ambalo tutajenga ‘Tanzanite
Exchange Centre’ ambayo kwa sasa tumefanya mazungumzo na wadau tutajenga kitu
kinaitwa ‘Tanzanite Smart City’ ambao utakuwa mji mkubwa wenye hoteli ndani yake,
Helikopta ambazo zitatua humo humo, ukumbi mkubwa wa mikutano wahusika hivi
sasa wapo Wizara ya fedha, likikamilika hili natamani siku moja mkutano mkubwa
wa madini ufanyike Mirerani,” amesema.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri
Mbibo ameongeza kuwa kupitia mnada huu uliozinduliwa leo, idadi ya wauzaji
waliojisajili kwenye mfumo wa kielektroniki wa kuendesha minada ni 195 wakiwemo
wafanyabiashara wadogo wa madini (brokers) 120, wafanyabiashara wakubwa wa
madini (dealers) 59, waongeza thamani madini (lapidary) 7 na wachimbaji madini
9. Kiasi cha madini kilicholetwa kwenye mnada ni kilogramu 184.06
kinachokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi za kitanzania bilioni 3.10.
Wakati huo huo akizungumza kwenye uzinduzi wa mnada huo
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mheshimiwa
Kilumbe Ng’enda amempongeza Waziri wa Madini kwa kuweka nguvu kubwa kwenye
utafiti wa madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania
(GST) na kuwezesha wachimbaji kuchimba bila kupoteza mitaji ikiwa ni sehemu ya
“Vision 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri,” na kuongeza kuwa,
“Kamati itaendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara lengo
likiwa ni kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini unakua na kufikia asilimia 10
ifikapo mwaka 2025.”
Naye Mbunge wa Simanjiro Mheshimiwa Christopher Ole
Sendeka amepongeza jitihada za Serikali kwa kupania kuleta mapinduzi ya
kiuchumi ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko na vituo vya ununuzi wa
madini nchini, kuhakikisha dhahabu inanunuliwa kupitia Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) hivyo kuendelea kuimarisha uchumi wa nchi.
“Ninashauri Serikali kuendelea kutilia mkazo wa biashara
ya madini ya vito kuendelea kufanyika katika mji wa Mirerani wakati ujenzi wa
Soko la Madini Mirerani ukiendelea,” amesisitiza.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga
ameongeza kuwa minada ya madini ya vito italeta manufaa makubwa kwa nchi ikiwa
ni pamoja na kukuza kipato kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini,
serikali kupata mapato, kuimarisha ubora wa madini ya vito na kuongeza ushiriki
wa watanzania katika Sekta ya Madini na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa za
uwekezaji katika Sekta ya Madini.



0 Maoni