Kikao cha Wajumbe wa Baraza la UNESCO la Jiopaki kilichofanyika
tarehe 10 Desemba, 2024 kwa njia ya mtandao kimeridhishwa na shughuli za
uhifadhi wa Jiolojia ya Ngorongoro Lengai ambapo NCAA imewakilishwa na Afisa
Uhifadhi Mkuu Dkt. Agness Gidna.
Tanzania kupitia Jiopaki pekee iliyoko kusini mwa jangwa
la Sahara ya Ngorongoro-Lengai (Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark) ambayo
inatambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, Sayansi na Utamaduni
(UNESCO) imepata kadi ya kijani (GREEN CARD) kama ishara ya umahiri katika
uhifadhi na utangazaji wa eneo lenye hadhi ya hifadhi ya Jiolojia (Geopark) kwa
kufuata masharti na miongozo ya UNESCO.
Kwa utaratibu wa UNESCO, maeneo yenye hadhi za Jiolojia
(Geopark) za UNESCO zinakaguliwa kwa kina kila baada ya miaka minne kwa ajili
ya kupima na kuona ufanisi na ubora kupitia shughuli mbalimbali zinazofanyika
katika maeneo hayo kwa kufuata vigezo vilivyoainishwa na UNESCO.
Hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro Lengai (Geopark)
inayosimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongroro ilipata hadhi ya kutambuliwa
na UNESCO Global Geoparks mwaka 2018, kutambuliwa huko kuliifanya kuwa Jiopaki
pekee kusini mwa jangwa la Sahara na jiopaki ya pili katika bara la Afrika
ikitanguliwa na M'Goun geopark ya nchini Morocco.
Katika tathmini na ukaguzi uliofanywa na wataalam kutoka
UNESCO mwaka 2022, hifadhi ya jiolojia ya Ngorongoro Lengai ilipata kadi ya
njano (Yellow Card), ambapo kwa miongozo ya UNESCO Ngorongoro Lengai ilitakiwa
kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza ndani ya miaka miwili ili kulinda hadhi
iliyopewa mwaka 2018.
Jitihada za serikali kupitia NCAA hasa katika uimarishaji
wa shughuli za uhifadhi, Ulinzi, kutangaza, kufuata masharti na miongozo ya
UNESCO katika kulinda hadhi ya eneo hilo ili kuendelea kuwa Hifadhi ya Jiolojia
inayotambulika kama “Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark” zilizaa matunda
baada ya timu ya UNESCO iliyokuja mwezi julai, 2024 kufanya uthibitishaji upya
(Revalidation) ambapo waliridhika na hatua zilizofanywa na Serikali katika
kufuata ,miongozo ya UNESCO katika eneo hilo.
Faida ambazo Tanzania itazipata kwa kuwa na kadi ya
kijani (GREEN CARD) ni pamoja na kuongezeka kwa muonekano chanya wa uhifadhi
kwa nchi ya Tanzania kimataifa, kuongezeka kwa idadi ya watalii na watafiti
watakaotembelea nchi ya Tanzania kwa Shughuli mbalimbali.
Faida zingine ambazo nchi inazipata ni pamoja na kupanua
wigo wa mashirikiano ya kimataifa katika sekta ya uhifadhi na utalii wa hifadhi
ya Jiolojia (Geopark) pamoja na kuongeza fursa ya kuongeza vivutio vingi vya
utalii na hasa utalii wa miamba.
Na. Kassim Nyaki- NCAA
0 Maoni