Jumla ya wananchi 97 waliokubali kuhama kwa hiari kutoka
ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera wilaya ya
Handeni Tanga, wametoa wito kwa wananchi wenzao waliobaki ndani ya hifadhi
kujiandikisha ili wapate uhuru na fursa ya kuboresha maisha yao nje ya Hifadhi
na kuepuka hatari ya kuishi na wanyama wakali katika eneo moja.
Wito huo umetolewa leo tarehe 19 Desemba 2024 na
wawakilishi wa wananchi hao ambapo kundi la 21 la awamu ya pili lenye kaya 23,
watu 97 na mifugo 196 limehama kwa hiari ndani ya hifadhi ya Ngorongoro
kuelekea Kijiji cha Msomera na maeneo Mengine waliyochagua wenyewe.
Bw. Daudi Melubo kutoka kijiji cha Kayapus ambaye ni
mmoja wa wananchi waliohama leo amesema yeye na familia yake waliamua kufanya
maamuzi ya kuhama ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kutokana na kutokua na
uhuru wa kujiendeleza kiuchumi kutokana na sheria za uhifadhi.
“Mimi nimeamua kuhama kwa hiyari yangu kwenda Msomera kwa
sababu huko kuna uhuru wa kujiendeleza, nitajenga nyumba, nitamiliki ardhi,
watoto wangu wataenda shule bila hofu ya mnyama na hakuna sheria kama
hifadhini, nawashauri ndugu zangu ambao bado hawajajiandikisha kuhama kwa hiari na watapata fursa ya kuendeleza na
kuboresha maisha yao,” alisema Daudi.
Kwa upande wake, Bi. Naishiye Sembeta alieleza kuwa; “Sisi
wanawake tumekuwa tukitembea umbali mrefu kwenda kutafuta kuni porini huku
tukihatarisha maisha yetu, ila sasa tunahamia Msomera na tunaamini maisha yetu
yatabadilika na kuwa bora zaidi.”
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi hilo, Meneja wa
mradi Afisa uhifadhi Mkuu Flora Asey amesema kuwa hadi kufikia leo tarehe
19/12/2024 jumla ya kaya 1,678 zenye
watu 10,073 na mifugo 40,593 zimekwisha hama ndani ya Hifadhi kuelekea Msomera
na wengine kwenye maeneo waliyochaguwa wenyewe.
Assey alisisitiza kuwa kwa sasa utaratibu uliopo ni
kuhakikisha kuwa zoezi la uandikishaji, tathmini ya maendelezo na uhamishaji
vinaenda sambamba ili kuhakikisha kila mwananchi anapojiandikisha anatumia muda
mfupi kuhama ndani ya hifadhi kwenda eneo alilochagua
Zoezi la kuhama kwa hiari ndani ya hifadhi ya Ngorongoro
linaendelea ambapo adhma ya Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha kuwa wananchi
hao wanapata fursa ya kuishi katika maeneo salama yenye huduma zote muhimu za
kijamii kwa ajili ya maendelea ya wananchi hao.
Na. Philomea Mbirika- NCAA

0 Maoni