Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa leo (Alhamisi, Novemba 7, 2024) amefanya ziara jijini Dodoma ili
kukagua utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwenye
taasisi zenye watu zaidi ya 100.
Waziri Mkuu
ametembelea kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Makutupora (834 KJ), shule ya
Sekondari Msalato na Gereza la Isanga ili kuona utekelezaji wa maelekezo ya
Serikali kuwa taasisi zote za Serikali na binafsi zinazotumia nishati ya kuni
kuandaa chakula cha watu zaidi ya 100 kwa siku zisitishe matumizi ya kuni na
mkaa kuwekeza katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo Desemba 31,
2024.
Akizungumza
na viongozi wa mkoa wa Dodoma na wa taasisi zote tatu kwa nyakati tofauti,
Waziri Mkuu aliwaeleza viongozi hao kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
alishatoa maelekezo na yeye anapita kuangalia kama wamebadilisha mifumo
inayotumika kwenye taasisi hizo.
“Nishati
safi ya kupikia ni ubunifu wa Rais wetu ambaye amebobea katika masuala ya
utunzaji mazingira, Rais wetu ametajwa kuwa ni kinara wa kampeni ya nishati
safi barani Afrika. Tusije kushangaa akiwa kinara wa kampeni hii duniani, kwani
ameshaenda Italia na Ufaransa kutoa mihadhara kuhusu nishati safi,” amesema.
“Kwa vile
Afrika na dunia inamtambua, Watanzania tusibaki nyuma, na ndiyo maana tuliunda
Kamati ya Kitaifa yenye wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. Wakati
kampeni hii inaendelea, tumetoa fursa kwa wajasiriamali kuanza biashara ya
kuuza mitungi ya gesi, mkaa mbadala na KUNIPOA kama njia ya kuwatoa wananchi
wetu kwenye nishati chafu ambayo ni kuni za kawaida na mkaa wa miti.”
Amesema
majeshi, polisi, vyuo vya elimu ya kati na ya juu, vyuo vya wizara mbalimbali
kama elimu, afya na kilimo ni baadhi ya maeneo ambayo yanapaswa kubadilisha
mifumo yao ya kupikia kwani yana idadi kubwa ya watumiaji vya vyakula.
Alitumia
fursa hiyo kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini, wafanye ukaguzi
kwenye taasisi zote hizo na wahamasishe wajasiriamali wanaopika chakula cha
watu wengi kama vile kwenye harusi ili nao waweze kubadilisha mifumo yao ya
kupikia. “Kupitia Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya wa Dodoma, ninawaagiza Wakuu
wa Mikoa na Wilaya kote nchini nendeni mkakague watu hao ili wabadilishe
teknolojia zao, ziendane na matumizi ya nishati safi ya kupikia.”
Amesema
ifikapo Desemba, mwaka huu wakuu hao watatakiwa watoe taarifa ya utekelezaji
ikionesha ni taasisi ngapi tayari zimetekeleza agizo hilo. “Tunataka ifikapo
Desemba, tujue taasisi ngapi tayari zimekamilisha, ngapi bado na mpango kazi
ukoje wa taasisi hizo. Tunataka ifikapo mwaka 2033, tuwe na asilimia 80 ya
Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia.”
Mapema,
akielezea utekelezaji wa programu hiyo kwenye makambi, Mkuu wa Jeshi la Kujenga
Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele alimweleza Waziri Mkuu kwamba wameanza
kutumia mfumo wa nishati safi kwenye vikosi vyote 26 vya JKT.
Alisema JKT
kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wanatekeleza mradi
utakaowapatia majiko banifu na sufuria zake 291 kwa vikosi vyote, majiko ya
gesi na sufuria zake 180, mitambo ya biogas tisa na majiko yake, mashine za
kutengeneza mkaa mbadala 60 ambapo mafunzo kwa vijana kuhusu mitambo hii
yataendeshwa na REA.
“Mradi wote
utagharimu shilingi bilioni 5.7 ambapo REA watatoa shilingi bilioni 4.34
(asilimia 76) na JKT itachangia sh. bilioni 1.38 sawa na asilimia 24.”
Naye, Mkuu
wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Msalato, Mwl. Mwasiti Msokola alisema
shule hiyo inatumia mkaa mbadala unaoitwa KUNIPOA ambao unatengezwa kwa kutumia
maganda ya miwa, miti na pumba za mazao.
Alisema
zamani walikuwa wakitumia sh. milioni 4.5 kila mwezi ili kununua kuni za
kawaida, lakini kwa sasa wanaokoa sh. milioni 1.3 kwa kutumia KUNIPOA.
Kwa upande
wake, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Jeremiah Katungu alisema Jeshi
hilo kwa kushirikiana na REA linatekeleza programu ya matumizi ya nishati safi
ya kupikia magerezani ambayo inahusisha vituo 211 ambapo kati ya hivyo magereza
ni 129, ofisi 26 za Magereza za Mikoa na Vyuo vya Magereza vinne.
Alitaja
vituo vingine kuwa ni Makao Makuu, Bohari Kuu, Hospitali kuu ya Jeshi,
Karakana, Shule ya Sekondari Bwawani, Kikosi Maalum na Kambi za Magereza 47.
Alisema
programu hiyo pia inahusisha utekelezaji wa miradi kadhaa ikiwemo ujenzi wa
mitambo 126 ya Biogesi, usimikaji wa mifumo 64 ya gesi ya LPG, ununuzi wa tani
865 za Mkaa Mbadala wa Rafiki; ununuzi wa mashine 61 za kutengeneza Mkaa
Mbadala unaotokana na Mabaki ya Mazao na kuimarisha matumizi ya gesi asilia
katika magereza ya Lilungu (Mtwara), Keko na Ukonga Complex (Dar es Salaam).
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu

0 Maoni