Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameelekeza kufikishwa mahakamani mara moja kwa maafisa wanne wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni na watumishi wanne wa kitengo cha Akaunti Jumuifu ya Amana (TSA) kilichopo TAMISEMI kwa tuhuma za ubadhirifu wa shilingi milioni 165.6.
Aidha, ameagiza Bi. Annie Nyabugumba
Maugo wa Kitengo cha Akaunti Jumuifu ya Amana asimamishwe kazi kutokana na
ushiriki wake kwenye muamala uliohamisha fedha kutoka TAMISEMI kwenda katika
Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni.
Ametoa maagizo hayo leo (Jumapili,
Oktoba 06, 2024) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya
Kigamboni, jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya
Wananchi. Waziri Mkuu yupo mkoani Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi ya siku
mbili.
Mheshimiwa Majaliwa amefikia maamuzi
hayo kutokana na uchunguzi uliofanywa na timu aliyoiunda kufuatilia tuhuma za
ubadhirifu huo pamoja na ukaguzi maalum uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ili
kujiridhisha na ukweli wa tuhuma hizo.
Waziri Mkuu amesema kuwa matokeo ya
timu ya uchunguzi aliyoiunda yalionesha kuwa watumishi hao walikuwa wanatumia
akaunti ya Amana kuficha fedha hizo tofauti na malengo ya matumizi ya akaunti
hiyo.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa
Septemba 05, 2022 watumishi watatu wasio waaminifu kutoka TAMISEMI
walishirikiana na watumishi kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kuleta
shilingi milioni 165.6 na kuzihifadhi kwenye akaunti ya Amana na zikakaa mwaka
mzima bila Mkurugenzi, Baraza la Madiwani na Wakuu wa Idara wengine kujua.
“Watu hawa wachache walikutana Dodoma,
wakati wa mapitio ya mahitaji ya fedha kwa ajili ya Halmashauri na
wakakubaliana na maafisa wa kitengo cha fedha za Halmashauri wa TAMISEMI, Bw.
Aidan Mponzi, Adora Mwombeki Mbalilaki na kukubaliana wataingiza fedha lakini
baada ya muda fedha hizo wazirudishe na fedha zikaingia na baada ya muda
wakaanza kufanya matumizi.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa
walianza kutumia fedha hizo bila kulijulisha Baraza la Madiwani na bila
kuingizwa kwenye bajeti ya Halmashauri ili wakuu wengine wa idara wajue kwamba
kuna fedha.
Ameongeza kuwa baada mtandao huo
kujulikana, timu ya uchunguzi ilifika katika Halmashauri hiyo na kumhoji
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Erasto Kiwale ambaye alikiri kutofahamu kuhusu
uwepo fedha hizo.
“Mkurugenzi alimuuliza Mkuu wa Kitengo
cha Fedha cha Halmashauri, Bw. Geofrey James Martin ambaye alikiri kuwepo kwa
fedha hizo na Mkurugenzi alimtaka
kuzirejesha zilipotoka kwa kuwa hazikuwa na maelezo ila Bw. Geofrey Martin hakufanya
hivyo na alipokuja kuhojiwa na timu ni kwa nini hakuzirejesha alisema fedha
hizo zimetumwa kwenye Halmashauri kwa ajili ya MDH (Management and Development
for Health) lakini hata Mganga Mkuu wa Wilaya hafahamu kama ameletewa fedha.”
Ameongeza kuwa Bw. Geofrey alipohojiwa
zaidi alikuwa muwazi na kukiri kwamba fedha hizo zimeletwa na watumishi wa
TAMISEMI kwa makubaliano kuwa sehemu ya fedha hizo zikishatumwa zirejeshwe kwa
Bw. Idan Zabron “Alieleza kuwa fedha hizo hazijatambulishwa kwa Baraza la Madiwani
kwa kuwa zilitumwa kinyume na taratibu.”
Amesema kuwa fedha hizo zilianza
kufanyiwa matumizi ambapo milioni 105.6 zikalipwa kwenye maboresho ya barabara
inayoelekea dampo la Lingate. “Fedha hizi zililipwa mara tatu, ambapo shilingi
milioni 77.5 alilipwa mzabuni anayeitwa Konya Investiment Company Ltd, shilingi
milioni 28.1 zililipwa kwa mzabuni anaitwa Mbogolo Investiment Company na
shilingi milioni 2.4 ilikuwa ni posho ya msimamizi.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa timu
ya uchunguzi ilipotembelea eneo la mradi na kumhoji mkuu wa mradi, Bw. Godwin
Adamson Cheyo ambaye alisema ujenzi wa barabara hiyo ulikuwa ni wa udongo
badala ya changarawe na gharama zote za mradi hazikuzidi milioni 30.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa timu
ya uchunguzi ilibaini barabara ilijengwa kwa udongo badala ya changarawe na gharama zote za mradi hazikuzidi milioni
30. Pia wazabuni waliotekeleza mradi hawakuwa na sifa na walitumika tu kupishia
fedha, na Bw. Jonathan Stanley Manguli ambaye ni Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya
ni mtia saini wa Kampuni ya Mbogolo Investiment Company na wanatumia anuani
moja na Konya Investiment Company Ltd” hivyo kuwepo na mgongano wa kimaslahi.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kwa kuwasimamisha kazi watumishi waliohusika na tuhuma hizo na wengine kufukuzwa kazi.
“Niwapongeze sana kwa kuchukua hatua,
na hasa Mkurugenzi unapokuja kupewa taarifa na ukajiridhisha kuwa fedha hizi
siyo stahili yetu ulishawaambia wazirudishe wao kwa kuwa walikuwa na mchezo
wao, hawakuzirudisha.”
0 Maoni