Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Kwa umma wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini - TAWA Beatus Maganja amesema taasisi ya TAWA imejipanga vyema katika kulinda maisha ya wananchi na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu nchini.
Maganja ameyasema hayo Oktoba 06, 2024
Katika Kijiji cha Igunguli kilichopo Kata ya Loje wilaya ya Chamwino Mkoani
Dodoma alipokuwa akitoa elimu kwa wakazi wa Kijiji hicho hususani wavuvi
wanaofanya shughuli zao katika bwana la mtera wakati wa ziara ya kutoa elimu ya
kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na
waharibifu.
"Sisi tumedhamiria, tumejizatiti
na tumejipanga kwamba tutasimama na wananchi kuhakikisha, kwanza tunawapa
elimu, lakini pia kulinda maisha yenu kwa kuendelea kufanya doria za mara kwa
mara ili kuhakikisha usalama wenu," amesema Maganja.
Akizungumzia hatua ambazo Mamlaka hiyo imekuwa ikichukua katika kukabiliana na changamoto ya mamba na viboko katika bwawa la mtera Maganja amesema TAWA imeimarisha doria zinazoshirikisha Askari wahifadhi na wanyamapori wa vijiji na kutoa elimu kwa jamii ya namna ya kujikinga na kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao.
Kufuatia jitihada hizo Maganja amesema
katika kipindi cha kuanzia Januari 2024 mamba watatu (3) na Viboko wawili (2)
waliokuwa hatarishi Kwa maisha ya watu na mali zao walidhibitiwa na zaidi ya
wananchi 300 wakiwemo wavuvi zaidi ya 40 walipatiwa elimu Katika vijiji
vilivyopo Kata ya Migoli.
Aidha, Afisa huyo amesema katika
kuimarisha ulinzi ya watu wanaoishi Kando ya Bwawa la Mtera, Mamlaka imeanzisha
kituo cha kudumu cha Askari Katika Kijiji cha Igunguli na Kijiji cha Migoli, kituo chenye jumla ya
Askari 20 ambao wamepatiwa vitendea kazi muhimu Kwa ajili ya udhibiti wa
wanyamapori wakali na waharibifu.
Katika hatua nyingine Maganja ametoa
rai Kwa wananchi kuendelea kufanya shughuli zao kama kawaida isipokuwa wachukue
hadhari wanapokuwa kwenye mabwawa, mito na madimbwi.
Vilevile amewasisitiza kuzingatia maelekezo
yanayotolewa na wataalamu wa uhifadhi ikiwemo kuacha kuoga au kufua ndani ya
bwawa na wavuvi kutumia nyenzo ZA kisasa katika shughuli za uvuvi huku
akiwataka kutoa taarifa kwa haraka Kwa wataalamu wa uhifadhi au Serikali za
vijiji husika ili hatua stahiki zichukuliwe Kwa haraka.
Naye Afisa Uelimishaji kutoka TAWA
Irene Bonaventure Midala amesema
Katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 Serikali imetenga bajeti ya ujenzi wa
Kizimba kimoja ambacho kitajengwa Katika Kijiji kimojawapo kati ya vijiji
vinavyozunguka bwawa la mtera lengo likiwa ni kupunguza changamoto ya
wanyamapori hao.
Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha
Igunguli wamepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA hususani
Kwa elimu wanayoitoa ambayo wanakiri imekuwa msaada kwao lakini pia mwitikio wa
haraka pale inapotokea changamoto ya wanyamapori hao.
0 Maoni