Wizara ya Maliasili na Utalii ya
Tanzania na Wizara ya Kilimo na Misitu ya nchini Finland zinakamilisha mradi
mpya wa kuboresha sekta ya misitu ili kuipa thamani sekta hiyo kuwa ya
kibiashara zaidi kutokana na uzoefu wa Finland.
Hayo yamebainishwa jana Oktoba 7,
2024, jijini hapa wakati wa kikao cha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na
Utalii ya Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi, na pacha wake katika sekta ya Misitu,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Misitu nchini Ufini (Finland), Bw. Pekka
Pesonen.
Dkt. Abbasi amesema Sekta ya misitu
imekuwa chanzo kikubwa cha ajira na Pato la Taifa la Finland ambapo kwa takwimu
za mwaka 2022 sekta hiyo iliingiza jumla ya Euro Bilioni 20 katika uchumi wa
Ufini hivyo Tanzania ina mengi ya kujifunza.
Ufini ambayo imekuwa ikitekeleza
miradi mbalimbali ya kusaidia sekta ya misitu nchini Tanzania ukiwemo Mradi wa
Forvac uliomalizika hivi karibuni uliochagiza ajira 500,000 katika sekta hiyo,
sasa iko tayari kusaidia mradi mwingine mpya kuendeleza mageuzi hayo.
“Kutokana na uzoefu wa wenzetu katika
biashara ya sekta ya misitu tayari tumekubaliana na tunakamilisha taratibu za
kuanza mradi mwingine mpya ambapo Finland itaisaidia Tanzania Euro milioni 20
kuchagiza mageuzi zaidi kuifanya sekta ya misitu kuisaidia Tanzania,” alisema Dkt.
Abbasi mara baada ya mkutano huo.
“Nimefurahia uzoefu mkubwa ambao
tumejadiliana na kupeana leo. Finland itaendelea kushirikiana na Tanzania na
sisi pia kuchukua uzoefu wenu katika kusimamia misitu hasa ya serikali kwani
hapa sisi uzoefu wetu mkubwa ni misitu ya sekta binafsi,” alisema Katibu Mkuu
huyo wa Ufini.
Awali kabla ya kukutana na Katibu Mkuu
huyo, Dkt. Abbasi na ujumbe wake walitembelea Kituo cha Kusimamia Sheria za
Misitu na pia Muungano wa Wazalishaji wa Kilimo na Wamiliki wa Misitu (MTK) wenye
wanachama 600,000.
Dkt. Abbasi ameongoza ujumbe wa
wataalamu ambao ni Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dkt. Deusdedit Bwoyo
na Kamishna wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos
Silayo.
Ufini ndio nchi inayoongoza Barani
Ulaya kwa kuwa na eneo lenye misitu mingi, sehemu kubwa (asilimia 60)
ikimilikiwa na sekta binafsi na asilimia kubwa inayobaki ikiwa chini ya umma
ikisimamiwa na kampuni binafsi ya Serikali ya Forestry LTD.
0 Maoni