Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha, kuvutia na
kuwakaribisha wawekezaji katika sekta ya madini ili kukuza uchumi wa mtu mmoja
mmoja na Pato la Taifa kwa ujumla.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia ametenga
kiasi cha shilingi bilioni 118 kwa ajili
ya kupeleka umeme kwa wachimbaji madini na kwa upande wa Kanda ya Ziwa
kuna maeneo zaidi ya 90 ambayo yanatarajiwa kupelekewa umeme.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Oktoba 5, 2024 mkoani Geita
wakati akifungua Maonesho ya Saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini.
“ Naomba nichukue fursa hii kuwashukuru tena Watanzania wote
kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika jitihada zake za kuendeleza sekta
mbalimbali za kiuchumi. Wajibu wa Serikali ni kuendeleza jitihada za
kujenga na kuimarisha misingi thabiti ya uchumi katika kuvutia wawekezaji kwenye
sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya madini, amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa lengo la Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ni
kuhakikisha sekta hiyo inafungamanishwa na sekta nyingine za kiuchumi ili
kuleta tija na maendeleo ya haraka kwa watu hasa kupitia ajira mbalimbali
zinazotokana na shughuli za utafutaji, uchimbaji, uongezaji thamani na biashara
ya madini nchini.
“Ili sekta ya madini iweze kuongeza mchango wake kwenye
uchumi wa nchi ni lazima ifungamanishwe kikamilifu na sekta muhimu za uchumi.
Ufungamanishaji wa sekta ya madini na sekta nyingine za uchumi ni dhahiri kuwa
utaliletea Taifa maendeleo kwa haraka kwa kuwezesha upatikanaji wa ajira pamoja
na kuchochea ukuaji wa uchumi,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, ametoa rai kwa Watanzania kujituma, kubadilisha mtizamo
na kuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea jitihada za Serikali za kuinua
uchumi wa nchi.
Pia, Dkt. Biteko ameipongeza Wizara ya Madini kwa jitihada
zake za kuanzisha uwepo wa akiba ya dhahabu, sambamba na kuipongeza Benki Kuu
ya Tanzania.
Akizungumzia kaulimbiu ya maonesho hayo ya madini kwa mwaka
2024 yenye ujumbe usemao “Matumizi ya
Teknolojia Sahihi na Nishati Safi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Endelevu.”
Dkt. Biteko amesema kuwa matumizi ya teknolojia na nishati
safi katika shughuli mbalimbali ikiwemo shughuli za madini hususan katika
utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani madini ni muhimu na
hayaepukiki.
“Katika kufanikisha hili matumizi sahihi ya teknolojia ni
muhimu sana ili kufanya shughuli za uchimbaji hasa zinazofanywa na wachimbaji
wadogo zifanyike kwa kuzingatia vifaa na teknolojia ya kisasa ili kufanya
uchimbaji wao uwe na tija na unaozingatia utunzaji wa mazingira,” amesisiza Dkt.
Biteko.
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa kwa sasa
bajeti ya wizara yake ni shilingi bilioni 232 kutoka shilingi bilioni 90
iliyokuwa awali ambapo wamejiandaa kujenga maabara kubwa ya kisasa ili
wachimbaji wapate fursa ya kufanya utafiti wa madini badala ya kwenda nje ya
nchi.
“Haya tunayafanya chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia
na ambaye ameelekeza kununua mitambo 15 ya uchimbaji madini ambayo tutaigawa
nchi nzima ikiwemo kwa vikundi vya uchimbaji vya akina mama na vijana,” amesema
Mhe. Mavunde.
Ameongeza kuwa mwaka
2017 sekta hiyo ilichangia asilimia 7.1 katika Pato la Taifa na sasa
inachangia kwa asilimia 9.0 huku malengo ikiwa ni asilimia 10 ifikapo 2025.
Amefafanua “Naamini ikifika mwakani tutafikia lengo kwa kuwa
vipo viashiria vinavyoonesha jambo hili linawezekana na malengo yetu kwa mwaka
huu wa fedha tutachangia shilingi trilioni 1 katika Mfuko Mkuu wa Serikali.”
Halikadhalika, Mhe. Mavunde amebainisha kuwa Serikali
inafanya jitihada mbalimbali za kutatua changamoto katika sekta ya madini na
kuwataka wachimbaji kuepuka migogoro
kwa kuzingatia Sheria ya Madini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine
Shigella amesema kuwa maonesho hayo yameshirikisha washiriki zaidi 800 na kuwa
Mkoa wake utaendelea kuboresha maonesho
hayo kuwa ya kitaifa.
Mhe. Shigella ameendelea kusema kuwa maonesho hayo yameleta maendeleo na mabadiliko makubwa na
kuwa ambapo kipindi cha uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia alifuta leseni ambazo
hazikuwa zinaendelezwa lakini kwa sasa Mkoa huo umetoa leseni kwa wachimbaji
wadogo zaidi ya 3,106.
Akitaja mafanikio ya sekta ya madini mkoani humo Mhe.
Shigella amesema “Tumewezesha wanawake kumiliki leseni 30 kwa vikundi zaidi ya
20 vyenye wanachama zaidi ya 1000. Geita inazalisha dhahabu angalau kilo 5000
kila mwaka na tayari shilingi trilioni 2.2 zimeingia kwenye mzunguko wa fedha.
Aidha, zaidi ya bilioni 65 zimetolewa
Serikalini kupitia madini katika mkoa wetu.”
Kuhusu uwepo wa nishati ya umeme katika maeneo ya wachimbaji
wadogo mkoani humo, Mhe. Shigella amesema tayari mkoa umepokea shilingi bilioni
7 na tayari miradi 52 inaendelea kutekelezwa ili kufikisha nishati ya umeme kwa
wachimbaji.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini, Mhe. Kilumbe Ng’enda amesema kuwa Kamati inaridhishwa na
kazi inayofanywa na sekta ya madini
ikiwemo namna inavyochangia Pato la Taifa pamoja na wachimbaji wadogo
kuchangia asilimia 40 katika pato hilo.
“Tunapongeza utulivu uliokuwepo katika sekta ya madini na
wachimbaji, sasa tunaipongeza Serikali na Waziri na tunaomba muendelee
kusimamia utulivu huu,” amesema Mhe. Ng’enda.
Vilevile, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji Madini Tanzania
(FEMATA), Bw. John Bina ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha sekta ya
madini nchini na kusema kuwa wachimbaji wa madini wote wameazimia kuendelea
kuiuzia Benki Kuu dhahabu kwa asilimia 20.
Makamu wa Rais wa Kambuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya
Geita (GGM), Simon Shayo amesema kuwa matumizi ya teknolojia sahihi kwa ajili
ya uchimbaji madini na nishati safi ni masuala yanaoungwa mkono na Kampuni yake
ambayo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza sekta ya madini
nchini.
“Tunafarijika kwa kuendelea kuwa wachangiaji kinara wa
mapato katika sekta ya madini na mafuta nchini Tanzania na tutaendelea kuwa mbia wa maendeleo,” amesema Bw. Shayo.
Manufaa ya Maonesho hayo yanatajwa kuwa ni kuwakutanisha
wadau na mifuko ya hifadhi ya jamii, kuongeza kipato katika mkoa, kuvutia
watembeleaji hadi kufikia 25,000, kukutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya
madini wakiwemo wafanyabiashara, wawekezaji, Vyama vya Wachimbaji Madini,
Mashirika ya Kimataifa na Asasi za Kiraia na washirikimbalimbali kutoka nje ya
nchi.
Awali akiwa Mkoani Geita, Dkt. Biteko amezindua nyumba sita za Maafisa wa Jeshi la Polisi zilizojengwa kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya Geita (GGM) mkoani kwa lengo la kuboresha makazi ya Maafisa wa Jeshi la Polisi pamoja na kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao.
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni