Mkuu wa wilaya ya Handeni Mkoani Tanga Mhe. Albert Msando amewahakikishia wananchi wanaoishi Tarafa ya Ngorongoro na wanataka kuhamia katika kijiji cha Msomera kutokuwa na hofu yoyote kuhusiana na maisha ndani ya kijiji hicho kwani ni salama na serikali imekuwa ikitatua kila aina ya changamoto inayojitokeza ili wananchi hao waweze kuishi kwa umoja,amani, ushirikiano na utulivu.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kijiji
hicho mwishoni mwa wiki Wakili Msando amesema kuwa tangu zoezi hilo kuanza
mwezi juni mwaka 2022 mpaka mwezi Septemba mwaka 2024 ameshapokea zaidi ya
wananchi 9,976 na mifugo 40,397 jambo
ambalo linaonesha wazi kwamba kadri wananchi wanavyoelimishwa wako tayari
kuhama.
DC Msando amewaambia wanahabari hao kuwa serikali ya Wilaya
ipo tayari kupokea makundi mbalimbali yanayotaka kufika katika kijiji hicho
ikiwemo waandishi wa habari, wanaharakati na asasi zisizo za kiserikali kutoka
ndani na nje ya nchi na kufanya kazi zao kwa uwazi ili waone kazi kubwa
iliyofanywa na serikali.
“Tunataka kukifanya kijiji cha Msomera kuwa cha mfano ambapo
dunia itakuja kujifunza namna haki za binadamu zionavyoheshimiwa na tunayafanya
haya ili kuwaondoa kwa hiari wananchi wetu wanaoishi katika Tarafa ya
Ngorongoro katika dimbwi la umaskini na changamoto mbalimbali wanazokabiliana
nazo ndani ya hifadhi ikiwa ni pamoja na kulinda maisha yao,” alisema Mhe.
Msando.
Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza kuwa hivi sasa dunia
inasisitiza kuhakikisha malengo ya milenia yanatimizwa ambapo kufikia mwaka
2030 kila mwananchi aweze kupata huduma zote muhimu za kijamii na ndicho
ambacho serikali ya Tanzania inakitekeleza kwa kuwahamisha wananchi kwa hiyari
kutoka Tarafa ya Ngorongoro kwenda Msomera na Maeneo mengine ambayo wananchi
hao watakayoyachagua.
Waandishi hao wa habari za uhifadhi wamempongeaa mkuu huyo
wa Wilaya kutokana na kazi kubwa aliyoisimamia katika kijiji hicho na kufanya
maisha ya wananchi kubadilika na kuwa yenye tija ambapo wananchi hao wameweza
kujengewa uwezo na kuanza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Katika ziara hiyo waandishi hao walitembelea katika Tarafa ya Ngorongoro na kujionea hali halisi ya mazingira katika eneo hilo pamoja na ongezeko kubwa la watu na mifugo ambapo walipofika katika kijiji cha Msomera wamejionea mabadiliko makubwa ya kiuchumi ya wananchi waliohama kwa hiari.
0 Maoni