WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka maafisa masuhuli
kwenye Halmashauri zote nchini waweke msisitizo wa kutumia mifumo ya
kielektroniki katika makusanyo badala la kukusanya kwa fedha taslimu ‘Cash’.
Amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza mapato katika
maeneo yao na kuepuka vishawishi vya kutumia vibaya fedha za umma ambazo
zinakusanywa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema hayo leo (Jumamosi, Oktoba 05, 2024) alipozungumza
kwenye kikao na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke jijini Dar es
Salaam. “Suala la mapato ni lazima mliwekee msisitizo ili tupate matokeo mazuri
kwenye halmashauri zetu. ”
Mheshimiwa Majaliwa pia ametoa wito kwa wakurugenzi wa
Halmashauri kutumia mapato ya ndani katika kutekeleza miradi ya maendeleo
badala ya kusubiri fedha kutoka Serikali kuu pekee.
“Acheni kutegemea mapato ya Serikali kuu pekee, tunataka
kuona mapato ya ndani yanatumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa umma
kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uaminifu ili mipango na malengo ya Serikali
ya kuwahudumia Watanzania yaweze kutimia.
Amesema kuwa watumishi wa umma ni wahudumu wa wananchi hivyo
wanapaswa kuwahudumia ipasavyo kwenye maeneo yao na kutatua kero zao. “Sisi
tunataka tuone mkifanya kazi kwa bidii, uadilifu, uaminifu usipofanya hivyo
utakuwa unakosa sifa za kuwa mtumishi wa umma” Amesema Waziri Mkuu.
“Sisi ni watumishi wa umma na ni wahudumu wa Wananchi,
tumefunga mikataba ili tuwe wahudumu wao, tumekubaki hilo, twende tukafanye
kazi, tunapaswa kuwatembelea walipo, kila mmoja ana wajibu wa kuwahudumia
wananchi kwenye maeneo yao. ”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa umma wafanye
tathmini ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika maeneo yao kwa kuangalia
hatua iliyofikiwa na sehemu iliyobaki ili mpaka kufikia June 2025 miradi hiyo
iwe imefikia zaidi ya asilimia 95 ya utekelezaji.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa umma
kusimamia maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na kutengeneza mazingira wezeshi
ya kujiendeleza kiuchumi. “Punguzeni
urasimu ili tujenge imani kwa tunao wahudumia, makundi yote yaliyo kwenye
maeneo yenu yakiwemo ya vijana, wazee, wanawake na wenye ulemavu lazima
tuwafikie na kusimamia uchumi wao.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa aliweka jiwe la msingi la uzinduzi wa bweni na bwalo kwenye shule ya Sekondari ya Kibasila iliyopo Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam ambapo amesema ameridhishwa na viwango vya ujenzi wa majengo hayo. Ujenzi wa miundombinu hiyo umegharimu shilingi bilioni 1.13
0 Maoni