Zoezi la Sensa ya Wanyamapori lazinduliwa leo Morogoro

 

Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mhe. Balozi, Dkt. Pindi  Chana amezindua rasmi zoezi la Sensa ya Wanyamapori  ikiwa ni kuhesabu Wanyamapori nchi nzima ili kuimarishs uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori, misitu ma kuendeleza utalii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi sensa ya wanyamapori  katika mfumo Ikolojia wa Nyerere - Selous - Mikumi ambao ni mfumo mkubwa nchini wenye kilomita za mraba 104,143, Waziri  wa  Maliasili  na  Utalii, Balozi. Dkt. Pindi Chana amesema Serikali imeendelea kuweka nguvu katika kuwahifadhi wanyamapori nchini.

"Zoezi hili linathibitisha jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori na misitu nchini na kuendeleza utalii," Mhe. Chana amesema.

Amesema Sensa hiyo katika ikolojia ya Nyerere - Selous- Mikumi  ni sensa ya 17 tangu kuanza kuhesabu Wanyamapori katika eneo hilo ambapo sensa itafanyika  kuanzia tarehe 5 Oktoba 2024 hadi Novemba 14, 2024.

Akizungumzia mchango wa  sekta hiyo kwa Taifa, Mhe. Chana amesema kupitia uhifadhi Sekta ya Maliasili na Utalii inachangia asilimia 21% ya pato la Taifa, asilimia 25% ya fedha za kigeni, kuzalisha ajira takribani milioni 1.6 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Amefafanua kuwa Sensa hiyo itahusisha maeneo ya hifadhi za Taifa za Nyerere, Mikumi, Mapori ya Akiba,  Selous, Lukwika-Lumesule, Liparamba na Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za Chingolie, Iluma , JUKUMU, Kisungule, Kimbanda, Mbaran'gandu, NALIKA-Tunduru, Ngarambe-Tapika, Liwale na Maeneo ya wazi yanayozunguka mfumo wa Ikolojia hiyo.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Dkt. Eblate Mjingo amesema sensa ya wanyamapori huonyesha viashiria ambavyo ni changamoto kwa wanyamapori na huisaidia Serikali kutenga rasilimali kwa ufanisi kukabiliana na ujangili, kuendeleza na kukuza utalii pamoja na kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori.

Zoezi hilo linafanyika kwa ushirikiano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zikiwemo TANAPA na TAWA chini ya uratibu wa TAWIRI.


Chapisha Maoni

0 Maoni