WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa
Washirika wa Maendeleo kushikiriana na Serikali katika kufanikisha utekelezaji
wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na kusaidia kuimarisha mfumo wa ugharamiaji
huduma za afya ili kuufanya kuwa endelevu.
Mheshimiwa Majaliwa amesema ili
kuimarisha mfumo wa ugharimiaji wa huduma za afya Serikali tayari imeanza
kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuendelea kuongeza kiwango cha bajeti ya
Sekta ya Afya.
Ametoa wito huo leo (Jumatano Oktoba
30, 2024) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika
ufunguzi wa mdahalo wa Bima ya Afya kwa Wote na Jukwaa la Kitaifa la
Ugharamiaji wa Huduma za Afya kwa ajili ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya
Afya kwa Wote (Universal Health Insurance - UHI), jijini Arusha.
“Pia, tumeanzisha mfuko kwa ajili ya
kugharimia wananchi wasio na uwezo, tumebainisha vyanzo mahsusi vya fedha kwa
ajili ya kugharimia Bima ya Afya kwa wananchi wasio na uwezo ambapo katika
bajeti ya mwaka 2024/2025 zimetengwa shilingi bilioni 173.5 kwa madhumuni hayo.”
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema
kuwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote utafanikiwa kutokana na uwekezaji
mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa
miundombinu na uborashaji wa huduma za uchunguzi.
Amesema Serikali imewekeza katika
ununuzi na usimikaji wa vifaa tiba vya kisasa vya uchunguzi na ugunduzi wa
magonjwa mbalimbali, ambapo hadi sasa zipo mashine za MRI 13, CT-Scan 45,
Digital X-Ray 346 na Ultrasound 668 kutoka 476 zilizokuwepo mwaka 2021. “Hatua
hii imewezesha kupatikana kwa huduma za kibingwa za uchunguzi.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa
Majaliwa amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa
dawa nchini kwa kutoa fedha kila mwezi kwa ajili ya ununuzi wa dawa.
“Hadi kufikia Oktoba 2024 upatikanaji
ulikuwa umefikia wastani wa asilimia 85 ambapo kwa upande wa zahanati ni
asilimia 76, vituo cha afya ni asilimia 75, Hospitali za Halmashauri asilimia
ni 78, Hospitali za Rufaa za Mikoa ni asilimia 99 na Hospitali ya Taifa, Maalum
na kanda ni asilimia 98.”
Kwa upande wake, Waziri wa Afya
Jenista Mhagama amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza
sana kwenye sekta ya afya kwa kuwa anatambua afya ni usalama, ulinzi wa Taifa na ni maendeleo ya Taifa.
Amesema kuwa katika kipindi cha
uongozi wa Serikali ya awamu ya Sita, sekta ya afya imeendelea kupewa
kipaumbele kwa kutengewa jumla ya shilingi trilioni 6.2 kwa ajili ya kutekeleza
shughuli mbalimbali zilizomwezesha mwananchi kupata huduma bora za afya karibu
na maeneo yao.
“Haya ni maamuzi ya kizalendo kwa
muktadha wa Taifa letu katika kutekeleza maono ya Baba wa Taifa ya kupambana na
maadui wa umaskini (maradhi).”
Naye, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la
Afya Duniani, Dkt. Charles Sagoe-Moses amesema Shirika hilo linaahidi kusaidia
utekelezaji wa Mpango Bima ya Afya kwa Wote lengo likiwa ni kuhakikisha
Watanzania wanapata huduma bora za afya kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Awamu
ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira ya
dhati ya kuanzisha mchakato wa Kitaifa wa Bima ya Afya kwa wote kama nyenzo ya
kufikia huduma za afya kwa wote.
“Utekelezaji wa Bima ya Afya ya Wote,
sio tu utakuwa na faida kwa afya ya Watanzania, bali itaacha alama katika
uongozi wake Tanzania na Afrika kwa ujumla kwa kuhakikisha Watanzania wanapata
huduma bora za afya.”
Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Washirika wa Maendeleo nchini Tanzania,
Moustafa Abdallah amesema kuwa watajitoa kusaidia safari ya Tanzania katika
utekelezaji wa mpango huo ili kuwawezesha Watanzania kupata huduma bora za afya
bila kujali uwezo wao wa kijamii na kiuchumi.
“Kwa kufanya kazi pamoja kati ya
Serikali, washirika wa maendeleo, watendaji wa sekta binafsi na wadau wote,
tunaweza kuhakikisha kuwa bima ya afya kwa wote inakuwa kweli, na
kuwahakikishia Watanzania wote afya bora.”
0 Maoni