Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameiagiza Wizara ya Mawasiliano na
Uchukuzi kuishughulikia Sheria ya vyombo vya barabarani na kuharakisha mchakato
wa kuwapatia wazee vitambulisho maalumu vitakavyowasaidia kulipa nusu nauli
kama ilivyo kwa wanafunzi na watu wenye ulemavu.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo
tarehe 7 Oktoba kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wazee, Duniani katika
ukumbi wa ZSSF, Tibirinzi Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameziagiza
taasisi zote za Serikali, zinazotoa huduma za usatawi kwa wazee, kuzishughulika
haraka na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wazee hao.
Taasisi zilizopewa maagizo hayo ni
Wizara ya Afya kuagizwa kuandaa madirisha maalumu hospitali zote kutoa huduma
bora za wazee kwa kuwapa kipaumbele, pamoja na kuongeza madaktari bingwa wa
magonjwa ya wazee.
Halikadhalika, Wizara ya Fedha
imeagizwa kuandaa bajeti maalumu ya kuendesha mabaraza ya Wazee pamoja na
kufungua madirisha maalumu kwenye benki na vituo vyote vinavyotoa huduma za
Fedha kuwapa kipaumbele wazee hao.
Rais Dk. Mwinyi amesema, Serikali
imeandaa na inaendelea kutekeleza Sera ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2014 ambayo
imeweka mikakati madhubuti ya kusimamia maendeleo ya wazee.
0 Maoni