Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa
ameitembelea Timu ya Taifa ya Tanzania ya Mpira wa Miguu (Taifa Stars)
inayofanya mazoezi kwenye uwanja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jijini Dar
es Saalm na kusema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassaan anamatumaini
makubwa kuwa timu hiyo itafanya vizuri kwenye michezo yote miwili.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo
(Jumatatu, Oktoba 07, 2024) alipozungumza
na wachezaji, benchi la ufundi pamoja na viongozi wakiwa katika
maandalizi ya michezo miwili ya kufuzu michuano ya AFCON 2025 dhidi ya Congo
itakayochezwa Oktoba 10 na 15, 2024.
“Kila mmoja aone ana jukumu kubwa,
kwako wewe mwenyewe na kwa nchi yako, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anawatakia
kila la kheri na alichofanya ametoa usafiri wa uhakika wa ndege itakayowapeleka
nchini Congo kwa ajili ya mchezo wa Oktoba 10, 2024, hili ni jambo kubwa.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kwa
jitihada za Rais Dkt. Samia amefanikiwa kushawishi mashirikisho ya mpira wa
miguu ya Afrika na FIFA ili kuiona Tanzania ni nchi ambayo imeamua kuboresha
viwango vya michezo ikiwemo mpira wa miguu. “Tumeanza kuona heshima tunayoipata
ya kuwa wenyeji wa baadhi ya mashindano ikiwemo CHAN.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa
amewataka wachezaji hao kushikamana, kuzungumza lugha moja na kutanguliza
uzalendo. “Tumieni fursa ya imani ya Watanzania kwenu kuiwakilisha vyema
Tanzania kwenye michezo iliyo mbele yenu.”
Kwa upande wake, Nahodha wa timu hiyo
Mohammed Hussein “Tshabalala” amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwezesha
kupatikana kwa usafiri wa ndege kwa ajili ya mchezo dhidi ya Congo. “Kwetu sisi
hii ni motisha kuelekea michezo yetu miwili dhidi ya Congo, kwasababu
itatusaidia kurejea haraka nyumbani kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa
marudiano.”
0 Maoni