Mavunde ashukuru wadau kuafiki mauzo ya 20% ya dhahabu BoT

 

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amewashukuru wadau wa madini, wachimbaji wakubwa, wa kati, wadogo na wafanyabiashara ya madini kwa kufikia muafaka wa kuwezesha utekelezaji wa kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini juu ya kutenga 20% ya uzalishaji wa dhahabu kwa ajili ya akiba ya nchi kupitia BoT.

Mhe. Mavunde amesema kwamba muafaka huyo umefikiwa katika kikao cha pamoja kati ya wadau wa madini na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Wizara ya Madini. “Tumefikia muafaka katika maeneo mengi na hivyo kuwezesha utekelezaji wa sheria hiyo.”

Akiongea leo Oktoba 7, 2024 Waziri Mavunde ametaja mambo muhimu waliofikia muafaka na wadau wa madini kuwa ni pamoja na bei itakayotumika ni bei ya dhahabu duniani kama inavyotolewa na Tume ya Madini. Bei hiyo hubadilika kila siku.

Pia, kufanyika kwa malipo ya asilimia 100 baada ya kupokea ripoti ya uchenjuaji wa dhahabu, ambapo muda wa malipo ni ndani ya saa 24 baada ya kupata ripoti ya uchenjuaji.

Kwa maana hiyo chini ya utaratibu huu wa malipo kwa miamala ya tarehe 02 Oktoba 2024, yalifanyika ndani ya masaa sita, amesema Waziri Mavunde.

Hali kadhalika, kwa upande wa gharama za kuchenjua dhahabu, Mhe. Mavunde ameeleza kuwa wamekubaliana Benki Kuu ya Tanzania italipia asilimia 100 ya gharama za kuchenjua dhahabu.

Mhe. Mavunde amefafanua kuwa kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini juu ya kutenga 20% ya uzalishaji wa dhahabu kwa ajili ya akiba ya nchi kupitia BoT kinamhusu mmiliki wa leseni ya chimbaji wa madini na mfanyabiashara mkubwa wa madini.

“Wafanyabiashara watapata motisha ya mrabaha asilimia 4 badala ya asilimia 6; Ada ya ukaguzi ni asilimia 0 badala ya asilimia 1; na Kodi ya Ongezeko la Thamani asilimia 0, hivyo muuzaji wa dhahabu anaweza kudai "input tax,” amesema Mhe. Mavunde.

Waziri Mavunde amemalizia kwa kusema kuwa chini ya mpango huu, wamiliki wa leseni ya uchimbaji wa madini, wafanyabiashara wakubwa wa madini na viwanda vya kuchenjulia dhahabu wanaweza kuiuzia Benki Kuu kiasi chochote cha dhahabu.

Chapisha Maoni

0 Maoni