Zaidi ya asilimia 90 ya huduma
zinazotolewa kwenye migodi ya madini nchini zinatolewa na Watanzania huku
vijana wakiaswa kutunza afya zao na kuepuka makundi hatarishi ili kuzifikia
fursa zilizopo kwenye migodi.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 7, 2024 na
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo wakati
akimwakilisha Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde kwenye ufunguzi wa
kongamano la mafunzo ya fursa katika Sekta ya Madini kwa vijana sambamba na
umoja wa vijana wa migodini (Tanzania Youth in Mining), kwenye ukumbi wa EPZA
uliopo viwanja vya Bombambili ambako Maonesho ya Saba ya Teknolojia na
Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini Geita yanayoendelea.
Mhandisi Lwamo amesema, Wizara ya
Madini kupitia Tume ya Madini imekuwa kinara kuhakikisha makundi yote
yanashiriki ipasavyo katika Sekta ya Madini ambapo imekua ikitoa leseni za
uchimbaji wa madini, vibali vya huduma kwenye migodi ‘local content’ na
kuongeza kuwa mpaka sasa hivi zaidi ya asilimia 90 ya watoa huduma ni Watanzania.
Amesema, Taifa lolote ili liendelee
linapaswa kuwa na vijana wenye malengo na tija na kuwataka vijana kuchangamkia
fursa zilizopo katika Sekta ya Madini ikiwemo fursa katika uchimbaji, fursa za
biashara na watoa huduma migodini ‘Local Content’.
“Fursa kama hizi ili muweze kuzifikia
ni lazima muwe kwenye vikundi na Serikali kupitia vikundi vyenu itaweza
kuwafikia na kutimiza lengo la vijana na kukuza uchumi kwa mtu mmoja mmoja na
nchi kwa ujumla,”amesema na kuongeza,
“Vijana, jambo kubwa na la msingi
niwaase ili kufikia ndoto zenu ni lazima mtunze afya zenu, mnaweza kuwa na
ndoto kubwa za mafanikio lakini kama afya zenu mnachukulia mzaha mzaha
hamtazitimiza tunzeni afya.”
Pia, amewaasa kuwa waaminifu kwa kuwa
vikundi vingi vya vijana vinakufa kutokana na kukosa uaminiufu.
“Tumeona vikundi vingi vinavurugika
wakati mwanga umeanza kuchomoza, mmetoka kwenye shida, imefikia wakati wa
kupata faida mnaanza kuleta vurugu kwenye vikundi, hatutaki vijana ambao mna
ndoto kubwa ya kutufikisha kwenye ‘Vision ya 2030’ ya Madini ni Maisha na
Utajiri mkaishia njiani, kwa kuingiza tamaa, kutokuaminiana ambako huzaa vurugu zisizo na faida,”amesema Mhandisi
Lwamo.
Aidha, amesema Serikali siku zote
imekuwa ikitoa kipaumbele kwa vijana kuhakikisha inaendelea kutoa leseni kwa
wachimbaji vijana ili wanufaike na rasilimali madini na kwamba ili kuendelea
kama taifa, kuna vitu vya msingi ambavyo vitapaswa kuzingatiwa ikiwemo kutunza
na kuendeleza maliasili ambazo Mwenyezi Mungu ametujalia.
“Tutaziendeleza kwa kuwa na elimu ya
kutosha ya kuendesha rasilimali hizi kibiashara, hivyo tumieni fursa za elimu
ya ujasiriamali ili muweze kufikia ndoto zenu kwa kunufaika na maliasili
zilizopo.”
“Sio wote mtachimba, naamini wapo
wenye vipaji vya uchimbaji, wengine biashara, kusambaza baruti, wengine
uchenjuaji wa dhahabu au madini yatakayopatikana, kila mtu ajiangalie kipaji
alichonacho akifanyie kazi kwa kuchangamkia fursa, Tume tupo kuwapa mwongozo
ili mfikie ndoto zenu, hivyo zingatieni mafunzo mtakayopewa hapa
hakikisheni hamtoki bure,”amesema Lwamo.
Awali akizungumza, Mwenyekiti wa Umoja
wa Vijana wa Madini Taifa, Hamis Mohamed amesema umoja huo uliundwa kwa
maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Rais Samia aliagiza tuunde umoja ili
changamoto zetu ziweze kutatuliwa kwa
urahisi pia tupate sehemu ya kusemea vitu vinavyotuhusu kama vijana katika
Sekta ya Madini ikiwemo kusaidiwa kuzifikia
fursa mbali mbali
zilizopo,”amesema Hamis na kuongeza,
“Wachimbaji vijana tuna changamoto nyingi,
Serikali haiwezi kututatulia changamoto zetu zote, zipo kupitia umoja wetu
tunakabiliana nazo na kuzitatua sisi wenyewe.”
Uzinduzi wa umoja huo wa vijana
umekwenda sambamba na mafunzo ambayo yametolewa na Mtaalam kutoka Tume ya
Madini, Mjiolojia John Maganga ambaye alimwakilisha Afisa Madini Mkazi wa
Geita, Samwel Shoo, ambapo amezungumzia fursa za kiuchumi, maadili kwa vijana
na kwamba dhamira ya Serikali ni
kuboresha maisha katika Sekta ya Madini.
0 Maoni