NSSF imejipanga kikamilifu kuifikia Sekta Isiyo Rasmi

  

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeamua kuja na mkakati maalum wa kuongeza wanachama wapya kutoka katika sekta isiyo rasmi, ili kuongeza wigo wa wanachama wake katika sekta hiyo inayokadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni 21.

Akiongea wakati akifungua mkutano wa NSSF na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Masha Mshomba amesema wanajua changamoto ya kuwafikia watu waliopo katika sekta hiyo ndio maana wamejipanga kuja na mkakati maalum.

“Sekta isiyo rasmi inachangamoto katika kuifikia ndio maana katika baadhi ya nchi ikiwemo nchi jirani ya Rwanda Serikali inatoa ‘incetive’ (motisha) kwa kuwachangia kiasi kidogo ili kuwahamasisha kujiunga na hifadhi ya jamii,” alisema Mshomba na kuongeza, “Na sisi tunafikiria pia kuongea na Serikali ili kuona hapo baadae kama itawezekana tuweze kuwa na motisha kwa kundi hili.”

Akiongelea Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo Rasmi ambayo ilianzishwa mwaka 2018, Mkurugenzi wa uwezeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Omary Mziya, amesema watafanya uzinduzi wa mpango huo hivi karibuni.

Bw. Mziya amesema kwa sasa wanalenga kuzifikia sekta za Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Uchimbaji mdogo wa madini, Sanaa mbalimbali, Biashara ndogo ndogo, Mama lishe/ Baba lishe, Bodaboda, Machinga na Wanahabari wa kujitegemea.

“Lengo letu ni kuongeza wigo kwenye hifadhi ya jamii na makundi yasiyonufaika na huduma hizo pamoja na kuchochea maendeleo na kasi ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla,” alisema Mziya.

Amesema NSSF imeweka mfumo rahisi wa kuchangia michango kwa wanachama walio katika sekta isiyo rasmi ambao unawawezesha kuchangia michango yao wakati wowote na wakiwa popote.

“Wanachama wa sekta isyo rasmi wanachangia mchango kiasi cha shilingi 30,000 kwa mwezi, ambapo kwa kutumia simu zao za kiganjani wanaweza hata kuchangia kidogo kidogo kiasi cha shilingi 1,000 ama 2000 kwa siku,” alisema Bw. Mziya.

Mziya amebainisha mafao kwa ajili ya makundi hayo kuwa ni mafao ya Pensheni ya Uzee, Mafao ya urithi, Mafao ya Ulemavu, ambayo ni ya muda mrefu na mafao ya muda mfupi ni Mafao ya Uzazi, Matibabu, Kujitoa kwa michango isiyozidi 50% au malipo ya mkupuo wa michango yote na msaada wa mazishi.

Ameeleza kuwa ili kupata fao la matibabu mwanachama anapaswa kuchangia kiasi cha shilingi 30,000 kutibiwa peke yake ama 52,000 kutibiwa mume/mke na watoto wanne. Pia mwanachama wa sekta isiyo rasmi anaweza kujitoa na kuchukua asilimia 50 ya michango yake ama kuchukua michango yake yote.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TEF Deodatus Balile ameipongeza NSSF kwa kuwekeza kwenye miradi yenye tija akitoa mfano wa daraja la Kigamboni ambalo limetatua changamoto ya usafiri kwa wakazi wa eneo hilo na kuchangia kuongeza thamani ya ardhi ya Kigamboni.

Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ina lengo la kuimarisha ustawi wa jamii kwa kuweka mifumo inayowakinga wananchi dhidi ya majanga ya kijamii yanayoathiri mapato (income) kama vile uzee, ulemavu, au kifo.

Chapisha Maoni

0 Maoni