Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) amesema, Mwenge wa Uhuru
umepandishwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro kusherekea Miaka 60 ya
historia yetu na kutukumbusha wajibu wetu wa kuhifadhi uhuru tulio nao kwa kujenga
Taifa lenye umoja, mshikamano, nguvu na maendeleo.
Mhe. Dkt. Stergomena, amesema hayo leo
tarehe 21, Oktoba 2024 katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Hifadhi ya
Taifa Kilimanjaro, wakati wa mapokezi ya kikosi maalumu cha Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) kilichopandisha Mwenge wa uhuru pamoja na bendera ya Taifa
katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Mhe. Dkt. Stergomena amenukuliwa
akisema, "Mwenge wa uhuru si tu alama ya ukombozi bali pia ni kielelezo
cha dhamira yetu kama nchi ya kuendelea kupigania amani, umoja na maendeleo ya
nchi yetu."
Akitoa pongezi kwa Jeshi la Wananchi
(JWTZ), Mkuu wa Jeshi la Ulinzi (CDF) Jenerali Jacob Mkunda, amekipongeza
kikosi hicho maalumu kilichopandisha
Mwenge wa Uhuru pamoja na Bendera ya Taifa katika Mlima Kilimanjaro kwa weledi,
uaminifu na uangalifu mkubwa wakiongozwa na Luteni Kanali Khalid Hamisi Khalid.
CDF Mkunda aliongeza, "Shukrani
za dhati ziwaendee uongozi wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kwa ushirikiano
mkubwa na ukarimu kwa timu nzima iliyopeleka Mwenge wa Uhuru na Bendera ya
Taifa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro."
Ikumbukwe kuwa tarehe 14, Oktoba 2024
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Rais Samia Suluhu Hassan
alimkabidhi Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Taifa Mkuu wa Jeshi la Ulinzi
Jenerali Jacob Mkunda, ili Jeshi hilo liupeleke kwenye kilele cha Mlima
Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya sherehe za miaka 60 tangu kuanzishwa kwa mbio
hizo za mwenge mwaka 1964.
Ambapo tarehe 15, Oktoba 2024 Kikosi maalumu cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) kilianza safari ya kupandisha Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Taifa katika
kilele cha Mlima Kilimanjaro kutekeleza agizo hilo na safari hiyo kuhitimishwa
rasmi leo tarehe 21, Oktoba 2024 kwa wanajeshi hao kurejea salama na wakiwa na
furaha isiyo na kitabı.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa serikali akiwemo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna wa Uhifadhi -
TANAPA, watendaji wa taasisi za serikali, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa
pamoja na viongozi wa Dini.
0 Maoni