WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Frank Chonya ahakikishe
mkandarasi anayejenga mabweni, madarasa na vyoo katika shule ya sekondari
Mandawa awe ameanza kazi ifikapo Oktoba 24, mwaka huu.
Akizungumza na walimu na wanafunzi wa
shule hiyo pamoja na viongozi wa Wilaya hiyo, leo (Jumatatu, Oktoba 21, 2024)
mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu hiyo, Waziri Mkuu
amesema kuwa Serikali imeamua kuipandisha hadhi shule hiyo kwa kuamua kuifanya
iwe na madarasa ya kidato cha tano na sita.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni
Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, yupo wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi ya siku
nne, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa sh. milioni 545 kwa ajili ya
ujenzi wa mabweni matatu, madarasa sita na matundu ya vyoo 12 katika shule
hiyo, iliyopo kata ya Mandawa, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Waziri Mkuu amekemea tabia ya
watumishi kupokea fedha za miradi na kukaa nazo huku wakifanya vikao bila
kufikia maamuzi yanayosaidia kuanza kwa utekelezaji wa miradi husika.
“Mmesaini mkataba Oktoba 8, mwaka huu,
lakini mpaka sasa hakuna kazi yoyote iliyofanyika, hivi kweli tutamaliza
majengo haya kwa wakati? Msingi wa bweni upo wapi? Tunataka ifikapo Desemba
mwaka huu, majengo yawe yamekamilika ili Februari, 2025 tuweze kuisajili,”
amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema kuwa msisitizo wa
Serikali ni kuona miradi yote inayoletewa fedha inakamilika na inaanza
kutumika. “Wananchi wanapoona mradi unajengwa, wanataka kuona mradi huo
unakwenda kwa haraka na kwa ubora ili ulete matokeo pale unapoanza kutumika.”
Akizungumza kwa nyakati tofauti na
wananchi kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika katika kata za Mandawa,
Namichiga na Matambarale, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kazi kubwa
inaendelea kufanyika katika sekta za elimu, afya, maji, umeme na barabara.
“Leo katika wilaya hii vijiji vyote
tumemaliza kuweka umeme na na sasa tunakwenda katika vitongoji. Tumemaliza
kujenga shule za msingi, huko hatuna shida. Kwa upande wa sekondari, tumepiga
hatua kubwa, kwani mwaka 2010 nilipoingia madarakani tulikuwa na shule tatu tu
za sekondari, lakini leo 2024 tuna shule 30 za sekondari, lengo ni kuona watoto
wa Ruangwa wanapata elimu mahali walipo.”
Akizungumzia kuhusu miundombinu ya
barabara, Waziri Mkuu amesema kuwa kwa sasa kuna mtandao wa lami wa kilomita 24
Ruangwa mjini. “Pia tuna mpango wa kujenga kilomita 100 za barabara za vijijini
kuelekea kwenye maeneo ya uzalishaji, ili kuongeza urahisi wa kufikisha mazao
sokoni; zote hizi tunaziweka lami.”
Kwa ujumla, Waziri Mkuu amewaomba
wakazi wa kata hizo waendelee kuwa watulivu na waendelee kuiamini Serikali yao.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi
wenzake, Kaka Mkuu wa shule ya sekondari Mandawa, Saidi Mohammed Mkowola
ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia kwa kutoa
fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni, matundu vya vyoo, vyumba vya madarasa
pamoja na ujenzi wa maabara ya kemia na bailojia na ununuzi wa vifaa vingi vya maabara.
Pia aliishukuru Serikali kwa kutoa
fedha kiasi cha sh. milioni 30 kwa ajili ya ukamilishaji wa maabara ya fizikia.
0 Maoni