Serikali kupitia Wakala ya Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) imekamilisha ujenzi wa daraja la Msadya lenye urefu
wa mita 60 na upana mita 10.5 pamoja na ujenzi wa barabara unganishi ya
Kibaoni-Chamalendi-Mdede kwa gharama ya shilingi bilioni 4.2 katika Halmashauri
ya Mpimbwe mkoani Katavi.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Mlele,
Mhandisi Paul Mabaya, ameishukuru serikali kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya
ujenzi wa daraja la Msadya lenye uwezo wa kupitisha magari tani 30 ambalo
limenufaisha wananchi wa kata za Mwamapuli, Chamalendi, Ikuba, Kibaoni na
Majimoto kusafirisha mazao yao.
“Daraja hili limekuwa mkombozi,
shughuli kubwa hapa ni kilimo na ufugaji, kiasi kikubwa cha mpunga unaolisha
nchi yetu unatoka maeneo haya ya Mwamapuli, Lunguya na Chamalendi kuna mashamba
makubwa ya mpunga na mahindi hivyo daraja hili limerahisisha usafirishaji wa
mazao na mifugo,” alisema.
Aliongeza kuwa Wilaya ya Mlele ina
Halmashauri ya Mlele na Halmashauri ya Mpimbwe, amemshukuru Rais Samia Suluhu
Hassan kwa kuongeza bajeti ya TARURA katika wilaya hiyo kutoka Bilioni 1 hadi
Bilioni 4 kwa mwaka na kwamba wanaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali
ili kuwezesha wananchi kuzifikia huduma za kijamii.
Naye, Mhe. Edward Madiliguntwe, Diwani
wa Kata ya Mwamapuli, ameishukuru serikali kwa kutengeneza daraja hilo
linalounganisha kata za Mwamapuli na Chamalendi ambalo limesaidia wananchi
kusafirisha mazao yao na kukuza shughuli za kibiashara na uchumi.
“Kata hizi zinategemewa sana kwa
kuzalisha chakula na kukuza mapato ya hapa na Halmashauri nzima, tunamshukuru
Rais Samia kwa kutuletea fedha za daraja hili ambalo limekuwa mkombozi kwetu,
zamani wananchi walipata shida kuvuka mto huu ambapo walikuwa wanavuka kwa
kubebana lakini sasa wanavuka bila shida yoyote,” alisema.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya
Chamalendi, Mhe. Yohana Maghembe alisema, kabla ya daraja hilo wananchi kutoka
Chamalendi ambao mahitaji yao yapo Majimoto kipindi cha mvua walikuwa wanapata
shida kuvuka na kupeleka mifugo yao mnadani eneo la Majimoto, baada ya daraja
kujengwa wananchi wanasafirisha mifugo, mazao na bidhaa zao kupeleka viwandani
na mnadani bila shida ambapo amemshukuru Mhe. Rais na ameomba TARURA iendelee
kuongezewa fedha ili barabara ziendelee kuboreshwa zaidi.
Naye, Bi. Jacquline Philipo mkazi wa
kijiji cha Mwamapuli alisema, wajawazito walikuwa wanapata shida kuvuka walikuwa
wanajifungulia njiani lakini sasa wanaishukuru serikali kwa kuwajengea daraja
ambapo kwa sasa wanafika hospitali kwa wakati.
Bw. Sylvester Kibigi mkazi wa Majimoto
amesema, kabla ya daraja kujengwa kipindi cha mvua pikipiki zilikuwa zinasombwa
na maji, kwasasa wanapita bila shida baada ya daraja na ameiomba serikali
kuendelea kuwaboreshea barabara kutoka darajani kwenda Mabambasi hadi Useja,
barabara ya Chamalendi-Sentakichaa na barabara kutoka darajani hadi Majimoto
ili ziweze kupitika katika nyakati zote.
0 Maoni