Mwezi mmoja baada ya ziara ya Rais wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini China, Tanzania
imefanikiwa kusaini Hati ya Ushirikiano ya uwekezaji na mafunzo na Kampuni ya
Huduma za Mawasiliano ya Kielekroniki ya China (CECIS LTD) utakaowezesha
kampuni zaidi ya 600 za vifaa vya Kompyuta kuwekeza nchini.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo
tarehe 21 Oktoba, 2024 na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis
Abdulla na Mwenyekiti wa Kampuni ya CECIS Bw. Guo Zhaoping na kushuhudiwa na
Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb).
Akizungumza mara baada ya kusainiwa
kwa hati hiyo Naibu Waziri Mahundi amesema uwekezaji huo utaongeza ujuzi kwa
vijana na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utengenezaji wa kompyuta na vifaa
vingine vya Kielektroniki utakaowezesha kupiga hatua kubwa katika masuala ya
uchumi wa kidijitali.
"Makubaliano haya ni matokeo ya
ziara ya Rais Samia nchini China aliyoifanya hivi karibuni, Kampuni hii ni
wabobezi wa masuala ya usalama wa mitandao hivyo elimu waliyonayo itawawezesha
vijana kujifunza kwani tunahitaji wataalamu wengi zaidi wa TEHAMA nchini,"
amesema Mhandisi Mahundi.
Akitoa salamu katika hafla hiyo Katibu
Mkuu Abdulla amesema uwekezaji huo utatoa fursa kwa watanzania kujifunza na
kupata ajira huku akiihakikishia kampuni hiyo ulinzi na usalama unaotokana na
uwepo wa sera na sheria nzuri kwa wawekezaji.
Bw. Abdulla amesema Tanzania ambayo ni
mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya
Kusini mwa Afrika (SADC), inayo fursa kubwa kwa wawekezaji kupata soko la zaidi
ya watu milioni 600.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni
ya huduma za mawasiliano ya kielekroniki ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa
Sayansi na Teknolojia wa Kamati ya Kampuni hiyo Bw. Guo Zhaoping amesema
uwekezaji huo umefuata misingi ya nchi za Tanzania na China na kwamba unalenga
kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali.
"Kampuni yetu inafanya uwekezaji
katika mambo makuu matano ikiwepo sekta ya kompyuta na usalama wa mitandao
ambapo pamoja na kufanya shughuli za kibiashara pia tunalenga kukuza uchumi wa
kidijitali baina yetu na nchi zingine, kwa hapa Tanzania tutafanya kazi
kulingana na mahitaji" amesema Bw. Zhaoping.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA
Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga amesema pamoja na mambo mengine, pia wamekubaliana
kuvutia kampuni mbalimbali za Kielekroniki kuwekeza nchini ambapo mwaka 2025
kutakuwa na maonesho makubwa ya utengenezaji wa vifaa vya kompyuta Afrika
ambapo Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Tume ya
TEHAMA watakuwa wenyeji wa maonesho hayo.
0 Maoni