Katika kuunga mkono jitihada za
Serikali katika ulinzi wa rasilimali za wanyamapori nchini, Kampuni ya Bushman
Safari Trackers iliyopo Mkoani Morogoro imetoa msaada wa pikipiki sita (6)
zenye thamani ya shilingi za kitanzania Millioni Kumi na tano (15,000,000) Kwa
Askari wa Uhifadhi wa TAWA kwa ajili ya kusaidia shughuli za doria katika Pori
la Akiba Maswa.
Akimkabidhi Kaimu Naibu Kamishna wa
Uhifadhi, Mlage Kabange msaada huo katika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA zilizopo
Mkoani Morogoro Oktoba 31,2024, Captain Willness Minja kwa niaba ya Kampuni ya
Bushman amesema wamekabidhi vitendea kazi hivyo kwa ajili ya kusaidia shughuli
za doria katika Pori la Akiba Maswa wao kama miongoni mwa wadau wakubwa wa
uhifadhi katika hifadhi hiyo.
Kwa upande wake, Kaimu Naibu Kamishna
Kabange ameishukuru Kampuni ya Bushman kwa ufadhili huo ambao unalenga
kuimarisha usimamizi wa shughuli za uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za
wanyamapori.
"Tunashukuru sana wawekezaji wetu
kwa msaada huu na vitendea kazi hivi vitaenda kuongeza nguvu na utarahisha
ufanyaji kazi wa doria, vilevile tunawaomba Bushman tuendelee kushirikiana
zaidi katika ulinzi wa rasilimali za wanyamapori," amesema Naibu Kamishna
Kabange.
Aidha, ameongeza kusema kuwa TAWA
inatambua mchango wa wawekezaji na
itaendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha rasilimali za wanyamapori
zinalindwa kikamilifu.
0 Maoni