Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
Upanga kwa kushirikiana na taasisi ya ROAD2IR ya nchini Marekani itafanya kambi
maalum ya uchunguzi na matibabu kwa wagonjwa wenye maumivu makali ya viungo na
sehemu mbalimbali za mwili kwa njia ya kisasa ya tiba radiolojia itakayoongozwa
na Daktari Bingwa Mbobezi wa matibabu hayo duniani Prof. David Prologo kutoka
Emory Health Care ya Marekani.
Tiba radiolojia ni aina ya taaluma ya
matibabu ambayo daktari bingwa mbobezi hutumia teknolojia ya picha za uchunguzi
za (Angio-Suite, CT, Xray, Ultrasound n.k) kumuongoza kufanya uchunguzi au tiba
kupitia matundu madogo mwilini bila kufanya upasuaji.
Dkt. Erick Mbuguje, Bingwa Mbobezi wa
Tiba Radiolojia MNH amesema, kambi hii itahusisha matibabu ya wagonjwa wenye
maumivu makali ya aina zote yaliyogawanyika katika makundi makuu mawili;
maumivu ya mgongo na maumivu ya sehemu nyingine za mwili.
DKt. Mbuguje amefafanua kuwa katika
kundi la kwanza ni wagonjwa wenye maumivu makali ya mgongo yasiyosababishwa na
saratani ni pamoja na pingili zilizosagika, kuvunjika au kupukutika ambapo
matibabu ya maumivu hayo hayahusishi upasuaji, diski zinazokandamiza mishipa ya
fahamu hivyo maumivu kusambaa sehemu za miguuni ambayo hayatibiki kwa upasuaji
na wagonjwa wenye maumivu yatokanayo na maungio ya pingili na kuongeza kuwa kwa
wagonjwa wenye maumivu ya mgongo yatokanayo na saratani iliyosababisha
kuvunjika kwa pingili au kubana kwa mishipa ya fahamu nao watahudumiwa.
Dkt. Mbuguje amesema kundi la pili ni
wagonjwa wenye maumivu makali ya viungo vingine vya mwili ambayo
hayajasababishwa na saratani kwenye magoti, mabega, nyonga ambayo matibabu ya
maumivu hayo hayaondolewi kwa njia ya upasuaji na kuongeza kuwa katika kundi
hili wenye maumivu mengine yatokanayo na saratani mbalimbali mfano kongosho nao
pia watanufaika na huduma hiyo.
Wagonjwa wote wenye changamoto hizo
wanaombwa kuwasiliana moja kwa moja na Dkt. Erick Mbuguje 0764497642, Dkt. Azza
Naif 0713264350 na Dkt. Mwivano Shemwetta 0755217298 ili kupata taarifa zaidi.
0 Maoni