TEF yapongeza uteuzi Bodi ya Ithibati ya Wanahabari

 

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limewapongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Tido Mhando na Wajumbe Ndugu Thobias Makoba, Ndugu Kingoba Mgaya, Dkt. Rose Reuben, Dkt. Egbert Mkoko na Ndugu Ladislaus Komanya kwa kuteuliwa kuunda bodi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na TEF leo pia imemumpongeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Slaa aliyefanya uteuzi huu jana Septemba 18, 2024 na kukamilisha kazi iliyokwamisha utekelezaji wa sheria hii tangu mwaka 2016, yaani miaka minane iliyopita.

Uteuzi huu ulioanza Septemba 18, 2024 utadumu kwa kipindi cha miaka mitatu.

Tarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile imesema, “Ni matumaini yetu kuwa kuteuliwa kwa Bodi ya Ithibati, kutaanzisha mchakato wa kuundwakwa Baraza Huru la Habari Tanzania (IMCT), ambalo sasa linakwenda kumaliza tatizo sugu la makosa ya kitaaluma kwa wanahabari kupelekwa mahakamani tofauti na taaluma nyingine nchini.”

“Tunaamini Mwenyekiti na wajumbe walioteuliwa wataifanya kazi hii kwa weledi mkubwa na kwa masilahi ya kukuza taaluma hasa katika kipindi hiki ambacho vyombo vya habari vinachangamoto kubwa ya uchumi,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imemalizia kwa kuwatakia kila la heri na kuwaombea katika kazi hii ambayo taaluma ya habari sasa inawekeza matumaini yote kwao.

Mungu ibariki taaluma ya habari, Mungu ibariki Tanzania

Chapisha Maoni

0 Maoni