Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imehitimisha kambi
maalum ya uchunguzi na upandikizaji wa meno bandia ambapo wagonjwa takribani 30
wamefanyiwa matibabu ya kupandikiza meno bandia kwa njia ya kisasa, huduma
ambayo imefanyika kwa mara ya kwanza katika Hospitali ya Umma nchini.
Kwa mujibu wa Bingwa wa Afya ya Kinywa na Meno Dkt. Peter
Shempemba zaidi ya wagonjwa 201 walifanyiwa uchunguzi katika kambi hiyo na
kubainika kuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutoboka au kuoza kwa meno,
magonjwa ya fizi, vibogoyo na mpangilio mbaya wa meno yao.
Dkt. Shempemba ameanisha kuwa baada ya uchunguzi huo kila
mmoja alipatiwa matibabu stahiki kulingana na changamoto walizonazo na kwa sasa
wanaendelea vizuri.
Dkt. Shempemba ameongeza kuwa takwimu zinaonesha kuwa asilimia
66 wanapoteza meno kwa sababu mbalimbali hivyo mahitaji ya kurudisha meno
yaliyopotea ni makubwa ndio maana hospitali hiyo imekuja na huduma hiyo
inayotumia teknolojia ya kisasa kabisa ili kuwasaidia Watanzania wengi kwa
gharama nafuu hapa hapa nchini.
Hospitali ya Taifa Muhimbili imeendela kuanzisha huduma za ubingwa bobezi ambazo hapo awali zilikuwa hazipatikani hapa nchini hivyo kuwapunguzia wananchi usumbufu na gharama za kwenda kutafuta matibabu hayo nje ya nchi.
0 Maoni