Maafisa wa Wakala wa Huduma za Misitu Kenya watembelea shamba la miti Sao Hill

 

Maafisa kutoka Wakala wa Huduma za Misitu nchini  Kenya wametembelea TFS - Shamba la Miti Sao Hill kwa ziara ya mafunzo ili kuona namna shughuli mbalimbali za uhifadhi zinavyofanyika ambao waliongozana na maafisa kutoka Wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabia Nchi na Misitu na mwakilishi wa JICA kutoka nchini Kenya leo Septemba 11, 2024.

Akizungumza kuhusu lengo la ziara hiyo ya siku mbili shambani hapo Naibu Mhifadhi Mkuu wa Uhifadhi Dr. Ng'oriareng P. Clement amesema kuwa wamekuja kujifunza namna shughuli mbalimbali zinavyofanyika ili kuona namna zitakavyowasadia katika shughuli za uhifadhi nchini Kenya.

Ameongeza kuwa wanaipongeza TFS kwa namna wanavyosimamia shughuli za uhifadhi ikiwa ni pamoja na utumiaji wa mifumo ya kisasa katika ukusanyaji wa mapato na utambuzi wa matukio ya moto na hivyo kufanya usimamizi wa rasilimali za misitu kwa ujumla kusimamiwa kwa tija.

Hata hivyo aliendelea kusema kuwa wameona namna shughuli zinavyofanyika ikiwa ni pamoja na uhifadhi wa misitu ya asili katika mashamba ya miti ya kupandwa ambayo inapelekea uhifadhi wa mazingira katika maeneo hayo kuwa endelevu na namna jamii inavyofaidika na uwepo wa msitu kwa kuwezeshwa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao, shughuli za ufugaji nyuki na uvunaji wa utomvu kutoka kwenye miti.

Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa TEHAMA kutoka TFS Harold G. Chipanha ambaye aliyemuwakilisha Kamishna wa Uhifadhi TFS wakati akiwakaribisha maafisa hao amesema kuwa TFS inasimamia mashamba 24 ya miti ya kupanda ambapo kati ya mashamba hayo Shamba la Miti Sao Hill ndilo shamba kubwa kuliko mashamba yote.

Amesema kuwa shughuli mbalimbali zimekuwa zikiendelea katika mashamba hayo  ya miti ya kupandwa ikiwa ni pamoja na upandaji wa miti ya kibiashara, uvunaji wa miti , ufugaji nyuki na utalii ikolojia na hii ni kutoka na shughuli nzuri za uhifadhi ambazo zinasimamiwa vizuri.

Aliongeza kuwa shughuli za uhifadhi zinafanywa vyema ni hii ni kutokana na kuwa karibu na jamii inayoizunguka misitu hiyo kwa kutoa elimu na kusaidia miradi mbalimbali ya maendekeo kama vile ujenzi wa madarasa , mabweni, madawati, barabara na utoaji wa huduma za afya katika vituo vilivyopo katika mashamba.

Ziara hii ya siku mbili inaendelea kesho Septemba 12,2024 kwa kutembelea bustani ya miche, eneo la muinuko ambalo linafahamika kama bahari ya miti, viwanda vikubwa na vidogo vya uchakaji wa mazao ya misitu.



Chapisha Maoni

0 Maoni