Wavuvi Musoma Vijijini wahamasika na mikopo nafuu ya Serikali ya uvuvi wa vizimba

 

Chama cha Ushirika cha Wavuvi wa Kitongoji cha Busumi (Busumi Fishing Cooperative Society) kimenufaika kwa kuchukua mkopo nafuu, usiokuwa na riba, kutoka Serikalini kwa ajili ya uvuvi wa vizimba ndani ya Ziwa Victoria.

Ushirika huu wenye wanachama 20 umekopa kiasi cha shilingi milioni 117 kwa ajili ya kupata vizimba vinne, vifaranga vya samaki, chakula na bima ya ufugaji wao wa samaki.

Taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini imesema wataalamu wa usukaji wa visimba wamekamilisha kazi zao na jana vizimba vilipelekwa ndani ya maji (Ziwa Victoria) eneo la Kijijini Suguti.

Uvuvi wa vizimba, kwa upande wa Jimbo la Musoma Vijijini, umeanza kwa mafanikio mazuri maeneo ya Vijiji vya Kigera (Etuma), Bwai Kwitururu na Suguti, imesema taarifa hiyo wa Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini.

Taarifa hiyo ya Mbunge wa Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo imesema kuwa wavuvi wa maeneo mengine wamehamasika sana na wanajitayarisha kutuma Serikalini maombi ya mikopo ya uvuvi wa vizimba.

Kwa upande wao wavuvi wa Musoma Vijijini wanaishukuru sana Serikali yetu chini cha uongozi mzuri wa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia mikopo mizuri isiyokuwa na riba, na kwa kuboresha uvuvi wao kwa kuufanya wa kisasa wenye mapato makubwa. 

Vizimba vya Chama cha Ushirika cha Kitongoji cha Busumi cha Musoma Vijijini vilivyowekwa ndani ya Ziwa Victoria vikiwa tayari kwa kuanza kufuga samaki.

Chapisha Maoni

0 Maoni