Wananchi waongeza kasi ujenzi wa Sekondari kata za Musoma Vijijini

 

Wananchi katika Jimbo la Musoma Vijijini wameongeza kasi ya ujenzi wa shule za Sekondari mpya za Kata kwa kushirikiana vizuri na Serikali.

Taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini imesema kuwa vilevile, kasi ya ujenzi imeongezeka pia kwenye ujenzi wa maabara tatu.

Maabara hizo tatu ni za masomo ya Sayansi (physics, chemistry & biology laboratories) ambazo zinajengwa kwenye kila Sekondari ya Kata.

Katika taarifa hiyo Mbunge wa Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo imesema mabadiliko mapya ya mfumo wa elimu nchini, yatahitaji ongezeko kubwa la shule za Sekondari.

“Mabadiliko hayo ni kwamba wanafunzi wa shule za msingi watasoma hadi darasa la sita (Std VI), na wote wataendelee kupata elimu ya Sekondari hadi Kidato cha Nne (Form IV),”imeeleza taarifa hiyo.

Jimbo la Musoma Vijijini lenye Kata 21, Vijiji 68 na Vitongoji 374, lina Sekondari za Kata na Serikali  26 na Sekondari za Madhehebu ya Dini mbili.

Taarifa hiyo ya Mbunge wa Musoma Vijijini imewasihi wananchi wa Musoma Vijijini kuendelea kuchangia ujenzi wa Sekondari mpya kwenye jimbo hilo.

Chapisha Maoni

0 Maoni