Ujerumani yasaidia mitambo ya kukarabati miundombinu Serengeti

 

Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA Musa Nassoro Kuji Juma leo Agosti 13, 2024 amepokea mitambo kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Frankfurt Zoological Society(FZS) kwa ajili ya ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara katika Hifadhi ya Taifa Serengeti. Mitambo hiyo itachagiza na kuongeza nguvu inayoendelea ya ukarabati wa miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua nyingi zilizonyesha mwanzoni mwa mwaka 2024 Kaskazini mwa Tanzania na nchi jirani ya Kenya.

Akipokea mitambo hiyo mitatu ambayo inahusisha “Motor Grader 2 na Roller Compactor 1” katika eneo la Fort Ikoma lililopo katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Kuji alisema, “Mitambo hii imefika kwa muda muafaka kutokana na wingi wa watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa sasa. Wingi huu wa wageni unaenda sambamba na wingi wa magari, ambayo husababisha njia zetu kuhitaji ukarabati wa mara kwa mara.”

Aidha, Kamishna Kuji aliongeza “Tunawashukuru sana FZS kwa msaada huu wa mitambo na niwahakikishie kuwa mitambo hii tutaitunza ili itumike kwa kazi iliyokusudiwa. Ni matumaini yetu kuwa miundombinu ikiimarika tutakuza utalii wetu na kufikia adhma ya Serikali ya kufikisha watalii milioni 5 na mapato ya dola za Kimarekani bilioni 6 ifikapo mwaka 2025. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeunga mkono juhudi za Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kukuza utalii na uhifadhi hapa nchini.” 

Naye, Mkurugenzi Mkaazi wa  Frunkfurt Zoological Society (FZS) - Tanzania ambao ni watekelezaji wa mradi huo wa Usaidizi wa Dharura kwa Uhifadhi wa Bioanuwai Tanzania - Dkt. Ezekiel Amani Dembe alisema, “TANAPA ni miongoni kwa wadau muhimu sana katika masuala mazima ya Uhifadhi na Utalii, hivyo tumekabidhi mitambo sehemu sahihi na salama, na tunawasihi kuitunza ili itumike kwa muda mrefu na kuendelea kukarabati na kufungua barabara zilizopo pamoja na barabara mpya kwa ajili ya utalii na shughuli za uhifadhi.”

Hata hivyo, Dkt. Dembe aliongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya TANAPA na Frankfurt Zoological Society (FZS) ni wa muda mrefu katika sekta ya uhifadhi na utalii hapa nchini na hivyo ni wajibu wa taasisi hizi mbili kuuendeleza ushirikiano huo kwa mustakabali wa uhifadhi endelevu nchini.

Kwa upande wake, Bw. Andrew Mwakisu ambaye ni Mratibu wa Mradi wa ERB kwa upande wa  FZS alisema, “Licha ya kukabidhi mitambo hii mitatu ili iendelee kuimarisha barabara za utalii katika hifadhi, pia mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti 2024 tutaleta mitambo mingine miwili ambayo tayari imeshafika nchini Tanzania ili kukamilisha jumla ya mitambo kufikia mitano (5) ambayo ndiyo iliyopangwa kununuliwa kupitia mradi huu.”

“Mitambo hiyo mingine miwili ambayo ni Excavator na Backhoe tayari imeshafika Jijini Dar es Salaam huku taratibu za mwisho zinaendelea ili kuifikisha mitambo hiyo katika Hifadhi ya Taifa Serengeti”, aliongeza Mwakisu.

Ikumbukwe kuwa Hifadhi ya Taifa Serengeti ndio hifadhi ya kwanza kuanzishwa nchini Tanzania ambapo ilianzishwa mwaka 1959 na ni moja ya hifadhi inayopokea watalii wengi zaidi kuliko hifadhi zote 21 zinazosimamiwa na TANAPA, ikikadiriwa kupokea zaidi ya watalii laki nne kwa mwaka.

Na. Brigitha Kimario- Serengeti

Chapisha Maoni

0 Maoni