Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara mijini na vijijini, na imepanga hivi karibuni kujenga barabara ya kisasa kuanzia Tunguu hadi Makunduchi yenye urefu wa kilomita 43.
Amesema barabara hiyo itakuwa na njia nne, taa, njia za
wapita kwa miguu, mitaro ya maji, pamoja na bustani.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 13 Agosti 2024, ikiwa
ni mwendelezo wa ziara yake ya kuzungumza na Wajumbe wa Kamati za Siasa za
Halmashauri Kuu ya CCM za Tawi, Wadi, Jimbo, Wilaya, na Mkoa wa Magharibi
kichama katika Ukumbi wa Mikutano, Viwanja vya Maonesho Nyamanzi, Dimani.
Aidha, Dk. Mwinyi amesema kuwa uwepo wa vyama vingi ni
kukuza demokrasia na siyo kuleta chuki na ubaguzi nchini, na amewataka
wanasiasa kuhubiri amani na kunadi sera za maendeleo kwa wananchi.
Vilevile, Dk. Mwinyi amewahimiza wanachama wa CCM
kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili kuwa na sifa ya
kushiriki Uchaguzi Mkuu mwakani na kukihakikishia Chama Cha Mapinduzi ushindi
wa kishindo.
Kwa upande mwingine, Dk. Mwinyi amewasisitiza viongozi wa CCM ngazi zote kunadi mafanikio ya Ilani ya Utekelezaji ya CCM 2020-2025 katika sekta mbalimbali zilizotekelezwa na Serikali kwa asilimia mia moja.
0 Maoni