Wizara ya Maliasili na Utalii imepongezwa kwa usimamizi mzuri wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) kwa kuwa Mradi huo ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania.
Pongezi hizo zimetolewa leo Agosti 13, 2024 na Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na
Utalii Jijini Dodoma, kwenye kikao maalumu kati ya Kamati hiyo na Uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa
lengo la Kamati kupokea na kujadili Taarifa za utekelezaji wa mradi wa REGROW
pamoja na Kanuni za Kifuta Jasho/Machozi.
Akijumuisha maoni ya Waheshimiwa Wabunge wa kamati hiyo,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb), licha ya kuipongeza
Wizara kwa kazi kubwa inayoifanya katika kukabiliana na changamoto mbalimbali
katika utekelezaji wa mradi, ameiagiza Wizara kuhakikisha inasimamia vyema Mradi
huo ili ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Mhe. Mnzava ameongeza kuwa, Mradi huo ni muhimu kwa
maendeleo ya Sekta ya Maliasili na Utalii, nchi pamoja na uchumi wa nchi hivyo
usimamizi madhubuti unahitajika ili ukamilike mapema kama ilivyopangwa ili
watanzania waweze kufaidi matunda ya uwepo wa mradi huo.
Aidha, Mhe. Mnzava amesisitiza kuwa, Wizara iendelee
kuchukua tahadhari kubwa kwenye utekelezaji wa mradi ili kuepusha vikwazo
vyovyote katika utekelezaji wa mradi kwa wakati.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki
(Mb) ameishukuru kamati hiyo kwa kuendelea kushirikiana na kuishauri Wizara
katika kutekeleza majukumu yake hali ambayo inachochea ufanisi kwenye
utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
Mhe. Kairuki ameihakikishia Kamati hiyo kufanyia kazi
maagizo yote yaliyotolewa na Kamati hususani la kuhakikisha kasi ya utekelezaji
wa mradi wa REGROW inaongezeka ili ujenzi unaoendelea ukamilike kwa wakati na
pia ameialika kamati hiyo kufanya ziara kujionea hatua za utekelezaji wa mradi
kwa sasa.
Aidha, kuhusiana na masuala ya kifuta jasho/machozi, Mhe.
Kairuki amefafanua kuwa Serikali hususan Wizara ya Maliasili na Utalii
inafedheheshwa na changamoto zinazosababishwa na wanyamapori wakali na
waharibifu na kuahidi kuendelea kufanyia kazi changamoto hizo na kupokea
ushauri wa kamati.
Pia amesema katika kukabiliana na changamoto hizo, Wizara
inaendelea kugawa mabomu ya kufukuza tembo katika Wilaya mbalimbali nchini
zinazokabiliwa na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu na imeweza
kuanzisha Mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji na uwasilishaji wa taarifa za
matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu [Problem Animals information
System-PAIS].
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imekutana na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kupata taarifa za utekelezaji wa mradi wa REGROW na kupitishwa kwenye Kanuni ya Kifutajasho na Kifutamachozi ya mwaka 2011 pamoja na marekebisho yake.
0 Maoni