Tanzania yatakiwa kujiimarisha kubaini maudhui ya upotoshaji mitandaoni

 

Kampuni ya Microsoft ya nchini Marekani imevishauri vyombo vya habari nchini pamoja na wadau wa maudhui ya kwenye mtandao kutilia maanani dhima ya uhalisi wa picha mnato, video na sauti kwa kufuatilia na kuthibitisha asili, historia na umiliki wake ili kutotumbukia kwenye upotoshaji unaofanywa kwa kutumia teknolojia ya Akili Mnemba.

Inaelezwa kwamba kuna umuhimu sana wa kuchukua tahadhari na hatimaye pamoja na hatua za kupambana na suala hilo kutokana na changamoto zinazotokana na teknolojia ya AI, hususan kwa kuibuka kwa baadhi ya watu wachache wanaotumia teknolojia hiyo kupotosha jamii (deepfakes).

Kwa kutambua changamoto hiyo ya uhalifu wa kimtandao ambayo pia inaweza kuleta mkanganyiko mkubwa hususan nyakati za uchaguzi, Kampuni ya Microdoft wametengeneza toolkits ambazo zitasaidia katika kubaini picha mnato, video na sauti zenye lengo la kupotosha jamii.

Hayo yameelezwa Mkurugenzi wa Mikakati na Usimamizi wa Biashara katika timu ya Democracy Forward ya kampuni ya Microsoft Bi. Amy Larsen kwenye mafunzo ya usalama wa uhalifu wa mitandao yaliyohudhuriwa na waandishi wa maudhui wa chama cha Mtandao wa Wamiliki wa Blogu Tanzania (TBN) na The CHANZO katika Kituo cha Marekani, Makumbusho ya Taifa, Mtaa wa Shaaban Robert, jijini Dar es Salaam.

Mtaalamu huyo ambaye anashika nafasi muhimu katika kusimamia mipango inayohusiana na usalama wa mtandao, taarifa potofu na habari za uongo, uadilifu wa uchaguzi, ulinzi wa uandishi wa habari wa ndani, na kukuza ushiriki wa kiraia wa kampuni, amesema mwaka wa 2024 na 2025 ni miaka muhimu kwa demokrasia na teknolojia, ikizingatiwa kuwa dadi kubwa ya watu kote ulimwenguni watapiga kura kwa ajili ya viongozi wao, huku maendeleo ya haraka ya AI yakileta fursa pamoja na changamoto kubwa kwa wakati mmoja.

“Hapa kuna sababu kwanini uhalisia wa maudhui ni muhimu katika mazingira ya sasa ya kiteknolojia, hususan katika kipindi hiki ambapo nchi nyingi zipo kwenye uchaguzi mwaka huu na hata hapa kwenu Tanzania mwakani pia mnao uchaguzi,” alisema Larsen.

Amesema moja ya wasiwasi mkubwa kwa sasa duniani ni matumizi mabaya ya AI kuunda "deepfakes" ni video, sauti, na picha bandia halisi ambazo zinaweza kudanganya wapiga kura kwa kubadilisha sura, sauti, au vitendo vya wanasiasa.

Bi. Larsen amesema ni lazima kupambana na taarifa za kupotosha kwani kuenea kwa maudhui yanayotokana matumizi ya AI, kama vile deepfakes, imekuwa rahisi zaidi watu wenye nia mbaya kuunda picha, video, na sauti bandia zinazoweza kupotosha na kudanganya watu kwa kuonekana kama ni za uhalisia.

Katika mafunzo hayo, Bi. Larsen aliangazia kwa kina mada ya Ushiriki wa Kiraia, Uelewa wa Vyombo vya Habari, Deepfakes, na Kuhusu Maudhui Katika Enzi ya AI, katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Marekani nchini Jijini Dar es Salaam.

Akiongelea hatua za haraka zinazochukuliwa kupambana na changamoto hiyo, Bi Larsen ameeleza kwamba kampuni 20 za teknolojia zimeungana kuanzisha mpango mpya uitwao Tech Accord to Combat Deceptive Use of AI in 2024 Elections, uliozinduliwa kwenye Mkutano wa Usalama wa mtandao mjini  Munich, Ujerumani, hivi karibuni. 

Amesema lengo kuu la makubaliano haya ni kupambana na matumizi ya deepfakes zinazozalishwa na AI ambazo zinaweza kudanganya maoni ya umma na kuhatarisha uadilifu wa chaguzi.

“Juhudi hii si ya upande wowote wa kisiasa na inaheshimu uhuru wa kujieleza, badala yake inalenga kuhakikisha wapiga kura wanafanya maamuzi sahihi bila kupotoshwa na taarifa za bandia zinazozalishwa na AI,” alisema Bi. Larsen.

Amesema juhudi hizo zitasaidia waandishi wa habari na mashirika ya vyombo vya habari ambavo hutegemea uaminifu na uadilifu, kuanzisha mnyororo wazi wa uhalisia, vituo vya habari vinaweza kuthibitisha kuwa picha na video wanazochapisha ni halisi na hazijabadilishwa.

Hii itasaidia kulinda uadilifu wa habari wanazotoa na kuhakikisha kuwa wasikilizaji wao wanaweza kuamini habari wanazopokea. Katika enzi ambayo habari za uongo ni tatizo kubwa, uhalisia wa maudhui unaweza kuwa kinga kwa viwango vya uandishi wa habari.

Bi Larsen ametoia wito kwa Tanzania kuwa macho wakati huu ambapo teknolojia za AI zinaendelea kukua, na umuhimu wa kubaini uhalisia wa maudhui ukiendelea kuongezeka.

Ipo haja kubwa kwa Tanzania kushiriki kikamilifu katika mpango huu mpya wa usalama mtandao wa  Tech Accord to Combat Deceptive Use of AI in 2024 Elections, ambao amsesema unatoa mfumo muhimu wa kuthibitisha uhalisia, kulinda dhidi ya taarifa za kupotosha, na kudumisha imani katika mwingiliano wa kidijitali.

“Kwa kuwekeza katika mifumo imara ya uhalisia, tunaweza kuhakikisha kuwa faida za AI zinatimizwa huku tukipunguza hatari zinazohusiana na matumizi mabaya ya teknolojia hii,”alisema Bi. Larsen.



Chapisha Maoni

0 Maoni