RPC Mbeya zindua kampeni ya kuwalinda watoto

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga akiwa ameambatana na watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mbeya amezindua Kampeni ya "Tuwaambie kabla hawajaharibiwa" ambayo imezinduliwa jana Kimkoa katika Shule ya Sekondari Mbeya day iliyopo Jijini Mbeya.

Akizungumza na Wanafunzi pamoja na Walimu shuleni hapo baada ya uzinduzi huo Kamanda Kuzaga ameeleza kuwa lengo la kampeni hiyo ni kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto.

Aidha, alisisitiza na kuwataka wanafunzi kutorubuniwa na kutofumbia macho vitendo vya ukatili ambavyo kimsingi vinakatisha ndoto za maisha ya wanafunzi badala yake kutoa taarifa za viashiria vya matukio ya ukatili kwa Jeshi la Polisi kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto, walimu, wazazi, walezi na hata pia kwa viongozi wa dini.

Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Mkoa wa Mbeya Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Veronica Ponera amesisitiza na kuwataka wanafunzi kutojihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwemo ubakaji, ulawiti pamoja na ushoga ambavyo hupelekea mmomonyoko wa maadili ya Kitanzania.

Sambamba na hilo, Msaidizi wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkaguzi wa Polisi (INSP) Lovenes Mtemi wa Dawati la Jinsia na Watoto ameeleza kuwa "Jukumu lenu ninyi kama wanafunzi ni kusoma hivyo mnatakiwa kuongeza juhudi katika masomo yenu ili kutimiza ndoto za maisha yenu ya baadae," alisema Mkaguzi wa Polisi Loveness.

Naye, Mkuu wa Shule ya Sekondari "Mbeya Day" Mwalimu Francis Mwakihaba amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa ushirikiano unaoendelea hususani katika utoaji wa elimu mbalimbali kwa wanafunzi katika Shule hiyo huku akiomba iwe endelevu kwani imekuwa ikisaidia sana kupunguza matukio ya Ukatili wa Kijinsia na Unyanyasaji dhidi ya Watoto.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa elimu mbalimbali kwa Jamii ikiwa na lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto huku likitoa wito kwa wazazi na walezi kutambua na kutimiza wajibu wao katika malezi ya watoto ikiwa ni pamoja na kuzungumza nao ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili na madhara yake.



Chapisha Maoni

0 Maoni