Katibu Mkuu wzara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amekakagua eneo la Mradi wa Samia Arusha AFCON City (SAAC).
Eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 4,555.5 lipo Kata ya Olmot
na Olasiti katika Jiji la Arusha na limepakana na miradi miwili ya viwanja
vitakavyotumika kwenye mashindano ya Afcon 2027.
Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya
mpira wa miguu ya Mataifa ya Afrika yatakayofanyika mwaka 2027 ambapo tayari
eneo litakalotumika kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa michezo hiyo limebanishwa.
Mhandisi Sanga ametembelea eneo hilo tarehe 28 Agosti 2024
jijini Arusha ikiwa ni jitihada zake za kuhakikisha mradi uliopangwa kutekelezwa
kwenye eneo hilo unatekelezwa kwa wakati ambapo Wizara yake imelekeza eneo hilo
kupangwa, kupimwa na kumilikishwa.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Arusha
Geofrey Mwamsojo, eneo hilo likipangwa litawekwa huduma muhimu zitakazowezesha
kuwa na mji nadhifu kulingana na matumizi yanayoendana na matumizi ya uwanja.
Amesema, Malengo ya mradi huo ni kuwa na mji nadhifu na
himilifu na unaojitegemea wenye huduma zote wezeshi kwa uwanja wa michezo,
kusaidia maendeleo ya Jiji la Arusha yanayofuata mpangilio bora wa makazi
pamoja na kuongeza wigo wa viwanja vitakavyojengwa Hotel za kitalii kwa ajili
ya Jiji la Arusha.
Mradi huo wa Samia Arusha Afcon City utatekelezwa kwa awamu
tatu ambapo awamu ya kwanza ni utwaaji vipande vya ardhi pamoja na uthamini wa
fidia ya vipande vya ardhi vitakavyoguswa na mradi, awamu ya pili kupanga eneo
zima la mradi lenye ukubwa wa ekari 4555.5, Kupima eneo lenye ukubwa wa ekari
180 ili kugawa viwanja pamoja na Kufungua miundombinu ya barabara kuu na za
ndani.
Awamu ya mwisho itakuwa endelevu na kuhusisha kazi za
umilikishaji wa viwanja, maandalizi ya hati na vikao vya kamati ya ugawaji wa
ardhi pamoja na usimamizi wa mradi utakao husisha utangazaji wa uuzaji wa
viwanja vya mradi.
Na. Munir Shemweta- WANMM
0 Maoni