Mwanaume aishi chini ya daraja kwa miaka 30

 

Kutana na mwanaume Liya’u Sa’adu ambaye ameishi chini ya daraja kwa miaka 30, kutokana na kushindwa kumudu gharama za maisha ya mjini.

Kwa kuishi karibu nusu ya maisha yake chini ya daraja kubwa Jijini Lagos nchini Nigeria, Liya’u Sa’adu anajiona kama mlinzi wa wenzake kadhaa wasionamakazi waliojiunga naye kuishi chini ya daraja.

Zaidi ya watu 30 sasa wanaishi na kulala nje chini ya daraja hilo la Obalende lenye harakati nyingi na kelele, kwa kushindwa kumudu hata kupanga kwenye vibanda.

Sa’adu amekuwa wakiwashauri wanaowasili, ambao mara nyingi ni vijana kutoka vijiji vya mbali jinsi ya kuishi mitaani katika jiji lenye kasi kubwa ya maisha ambayo ni rahisi kujiingiza kwenye uhalifu.

“Nina umri wa miaka 60 na kuna vijana waliokuja hapa miezi iliyopita ama miaka michache iliyopita. Naona kuwa ni jukumu langu kuwaongoza,” Sa’adu ameiambia BBC.

“Ni rahisi mno kupoteza mwelekeo Jijini Lagos, hususan kwa vijana kwa kuwa wanakuwa hawana familia ya kuwaangalia mienendo yao.”

Kama ilivyo kwa watu wengi wanaoishi chini ya daraja hilo Sa’adu anazungumza lugha ya Hausa, lugha ambayo inazungumzwa na watu wengi eneo la kaskazini mwa Nigeria.

Sa’adu aliwasili Lagos akitoke mji mdogo wa Zurmi kaskazini magharibi mwa jimbo la Zamfara mwaka 1994, ambapo marafiki zake wote ama wamekufa ama wamerejea vijijini kwao.

Chapisha Maoni

0 Maoni