Kamishna Kuji aipongeza kampuni ya “TIL” kwa ukarabati wa barabara

 

Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Nassoro Juma Kuji, leo tarehe 23.8.2024 ametembelea na kufanya ukaguzi wa Mradi wa Ukarabati mkubwa wa barabara kutoka lango la  Ngongongare, Momella mpaka lango la Nasula yenye urefu wa Kilomita 16 unaotekelezwa katika Hifadhi ya Taifa Arusha na Kampuni tanzu ya TANAPA Investment Limited (TIL).

 Akikagua Mradi huo ambao ni mhimili mkubwa kwa utalii katika Hifadhi hiyo, Kamishna Kuji aliridhishwa na kiwango kizuri cha mradi huo sambamba na hatua ya ukamilishaji iliyofikiwa na kuipongeza Kampuni ya TIL kwa kuanza utekelezaji wa mradi huo ndani ya Shirika kwa kiwango cha ubora unaokubalika na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD).

 “Nimeridhishwa na kazi hii ambayo imefanywa na TIL. Hii ni Hifadhi ya kwanza kunufaika na miradi iliyopangwa kutekelezwa na kampuni yetu. Ukamilishwaji wa barabara hii utachochea kwa kiasi kikubwa ongezeko la watalii na mapato na hivyo kutimiza malengo ya Ilani ya Chama Tawala ya kufikia watalii milioni 5 na mapato ya Dola za Kimarekani bilioni 6 ifikapo 2025 ,”alisema Kamishna Kuji.

Naye, Msimamizi Mkuu wa TIL Mhandisi Dkt. Richard Matolo, amesisitiza kuwa Kampuni imejizatiti vya kutosha katika kuboresha miundombinu ya Shirika kwa viwango vinavyokubalika.

“Huu ni mradi wetu wa kwanza ndani ya TANAPA, tumeanza hapa, na tunatarajia kukamilisha ndani ya siku tano kwa kuzingatia ubora wa hali ya juu. Baada ya hapa, tutaelekea Hifadhi ya Taifa Serengeti ambako tutaanza na barabara ya Golini - Naabi mpaka Seronera yenye urefu wa Kilomita 68, na baadaye kuendelea na barabara zingine kuhakikisha kuwa Serengeti inaendelea kuwa Hifadhi Bora barani Afrika, ”alisema Dkt. Matolo.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Eva Mallya ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha amelishukuru shirika kwa kuwezesha uboreshaji wa miundombinu ya barabara hifadhini  kwani itapelekea watalii hifadhini kuendelea kuongezeka kwani miundombinu yake inakuwa rafiki kwa magari makubwa na hata yale madogo na kuahidi kuendelea kusimamia matumizi sahihi ya barabara hizo ili kutimiza adhma ya serikali ya kufanya maboresho hayo.

Ukarabati wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 16 kwa kiwango cha Changarawe umegharimu kiasi cha shillingi Millioni 411.



Chapisha Maoni

0 Maoni